Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Singida FG yatimua kocha wa tatu

Ricardo Ferreira Fh Kocha Ricardo Ferreira

Thu, 28 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Singida Fountain Gate (SFG) imeachana na kocha mkuu Ricardo Ferreira aliyedumu kwa miezi miwili tangu Oktoba 15.

Akizungumza nasi, Ferreira alieleza mambo yalianza kuonekana mabaya Desemba 21 wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Geita Gold walikopoteza kwa bao 1-0.

“Ni kweli nimesitishiwa mkataba na Singida na nilianza kupewa taarifa kupitia wakala wangu aliyeambiwa na rais wa klabu, Japhet Makau. Hivyo kwa sasa najiandaa kurudi Brazil,” alisema.

Mwanaspoti lilimtafuta mtendaji mkuu wa klabu hiyo, Olebile Sikwane kuzungumzia suala hilo aliyesema kwa sasa hawezi kuzungumza chochote kwani mipango yao ipo katika michuano ya Kombe la Mapinduzi inayoanza leo Zanzibar.

Ferreira aliyesaini mkataba hadi Julai mwakani ameiongoza Singida katika michezo tisa ya ligi akishinda minne, sare tatu na kupoteza miwili akiiacha nafasi ya tano na pointi 20.

Mbrazili huyo anakuwa kocha wa tatu kuondoka baada ya Mholanzi Hans Van de Pluijm aliyeiongoza kufuzu hatua ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-3 dhidi ya JKU baada ya awali kushinda 4-1 huku Ligi Kuu akiiongoza kwa mchezo dhidi ya Tanzania Prisons ulioisha kwa suluhu.

Baada ya Hans, kuondoka Singida ikamtambulisha Mjerumani Ernst Middendorp Septemba 1 aliyeondoka Septemba 19 akiiongoza katika mchezo mmoja wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Future ya Misri akishinda bao 1-0. Kwa sasa ipo mikononi mwa Thabo Senong, raia wa Afrika Kusini.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live