Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Singida FG yasaini mkataba wa ushirikiano na Sekhukhune United

Wdewre Singida FG yasaini mkataba wa ushirikiano na Sekhukhune United

Thu, 4 Apr 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Klabu ya Singida Fountain Gate imesaini mkataba wa ushirikiano na klabu ya Sekhukhune United inayoshiriki Ligi Kuu Afrika Kusini (PSL).

Mkataba huo umesainiwa na Rais wa Klabu ya Singida Fountain Gate FC, Japhet Makau na Mwenyekiti wa Klabu ya Sekhukhune United, Simon Malatji.

Akizungumza na Mwanaspoti, ofisa habari wa klabu hiyo, Hussein Massanza amesema mkataba huo hauna ukomo na pia umejikita katika sehemu nne za ushirikiano ambazo ni ufundi, Biashara ya wachezaji, Kukuza soka la wanawake na vijana pamoja masuala ya uendeshaji wa klabu.

“Ushirikiano wetu hauna ukomo, utakuwa katika sehemu nne ambazo ni sehemu ya kiufundi ambapo hapa tulianza mapema mkuu wa ufundi wa klabu hiyo alikuwa na sisi kipindi cha Mapinduzi Cup hata pia tulipocheza na Simba.

“Tutajikita kwenye biashara ya wachezaji hapa tutauza na kununua wachezaji katika timu hizi au pia kuchukua kwa mkopo,” ameongeza Massanza.

“Tutashirikiana pia katika kukuza soka la vijana pamoja na soka la wanawake ambapo wenzetu hawa wamefika mbali katika eneo hilo, hata wachezaji wetu vijana watapata nafasi ya kucheza soka nje, sehemu nyingine ni katika uongozi na uendeshaji wa kisasa wa klabu ambapo Sekhukhune walikamilisha hilo miaka kumi nyuma, hivyo tutajifunza mengi kupitia wao,” amesema Massanza.

Huu sio mkataba wa kwanza wa ushirikiano klabu hiyo inasaini, Singida FG walishasaini mkataba na US Monastir ya Tunisia pamoja na Mafunzo FC ya Zanzibar ambapo Massanza anasema urafiki wao bado upo, unaendelea vizuri na muda si mrefu yataonekana matunda yake.

Sekhukhune FC ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Afrika Kusini ikiwa imecheza mechi 21 na kuvuna pointi 34 ikishinda mechi 10, sare 4 na imepoteza mechi 7 ikiongozwa na Mamelodi Sundowns iliyopo kileleni na Stellenbosch ipo nafasi ya pili.

Singida FG kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ipo nafasi ya 7 ikicheza mechi 21 na kuvuna pointi 24, ikishinda mechi 6, droo 6 na imepoteza mechi 9.

Mapema wiki hii Makau alisafiri kuelekea nchini Afrika Kusini kukamilisha mchakato wa kusaini makubaliano hayo.

Chanzo: Mwanaspoti