Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Singida FG yaanza na kocha mpya

Singida FG Singida FG yaanza na kocha mpya

Sun, 2 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Uongozi wa Singida Fountain Gate umeanza kufanyia tathimini ya kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao huku kipaumbele cha kwanza ni kuhakikisha inampata kocha mzuri baada ya msimu huu kuandamwa na jinamizi la kuondoka kwa makocha wengi.

Taarifa kutoka ndani ya timu hiyo zililiambia Mwanaspoti, viongozi wameanza vikao kwa ajili ya kujadili mwelekeo wa msimu ujao huku mbali na ishu ya kocha jambo lingine linalopewa uzito mkubwa ni usajili wa nyota wapya.

Makamu wa Rais wa timu hiyo, John Kadutu aliliambia Mwanaspoti wanataka kutengeneza kikosi imara ingawa mipango kwa sasa bado ni mapema kuiweka wazi. “Siwezi kusema tutafanya nini lakini tuna malengo ambayo sisi kama viongozi tumeyaweka na tutayafanyia kazi baada tu ya msimu huu kuisha. Kwa sasa mashabiki na wadau wetu wakubwa waendelee kutusapoti kwani mambo mazuri yanakuja,” alisema Kadutu.

Tayari timu hiyo iko mbioni kumpoteza beki wa kushoto, Nickson Kibabage aliyepo Yanga kwa mkopo wa msimu mzima ingawa mazungumzo ya kumsajili moja kwa moja yanaenda vizuri na Singida imeanza kutafuta mbadala wake atakayeziba nafasi yake.

Mbali na nafasi ya Kibabage, pia wanaangalia namna nzuri ya kuboresha eneo la kiungo mkabaji baada ya nyota wa timu hiyo, Yusuph Kagoma kukaribia kujiunga na Yanga, huku dili hilo likiwa mwisho kukamilika akitajwa kama mbadala wa Khalid Aucho.

Tofauti na maeneo hayo, jingine ni la kumpata kocha mkuu kwa ajili ya msimu ujao ambaye atatoa mapendekezo ya sehemu nyingine za kuboreshwa ikitegemea na wachezaji waliopo kama wengine wataondoka au wataendelea kubaki.

Mchakato wa kocha unachukuliwa kwa uzito mkubwa kwani haitaki kutokea yaliyotokea msimu huu baada ya kuondoka kwa makocha watano. Makocha hao ni Hans Van de Pluijm, Ernst Middendorp, Ricardo Ferreira, Thabo Senong na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’.

Baada ya kuondoka kwa Julio timu hiyo ilikabidhiwa kwa Ngawina Ngawina aliyekuwa anaifundisha FGA Talents inayoshiriki Ligi ya Championship, jambo ambalo vigogo hao hawataki tena kuona linajirudia msimu ujao ili kutengeneza kikosi imara.

Ngawina aliyepewa mkataba wa kuinoa timu hiyo hadi mwisho wa msimu, amekiwezesha kikosi hicho kumaliza nafasi ya 11 na pointi 33 katika Ligi Kuu Bara ingawa bado viongozi hawajafanya maamuzi ya kumkabidhi moja kwa moja kwa ajili ya msimu ujao.

Chanzo: Mwanaspoti