Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Singida FG waliwezaje?

Singida FG Future FC Singida FG waliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Future FC

Thu, 21 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baada ya wawakilishi wetu wawili waliokuwa ugenini kwenye michuano ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kutafuta nafasi kuingia makundi kwa Simba kulazimisha sare Zambia dhidi ya Power Dynamos na Yanga kupata ushindi Rwanda dhidi ya El Merreikh michezo ikichezwa siku ya Jumamosi.

Jumapili ikawa zamu ya wawakilishi wetu kwenye Kombe la Shirikisho la Afrika, Singida Fountain Gate walipocheza na Future FC ya Misri nao wamepata ushindi wa bao moja bila .

Ulikuwa ni mchezo mkali wenye mvuto pamoja na kuwa timu zote ni ngeni kwenye michuano hii, lakini zilicheza kwa kasi kuanzia mwanzo hadi mwisho.

MASHABIKI NJE YA UWANJA

Ungeweza kufikiri timu iliyokuwa inacheza ni kati ya timu hizi kubwa mbili yaani Simba na Yanga jinsi mashabiki walivyokuwa wengi ndani ya Azam Complex. Ilitosha kuwa silaha kubwa kuufanya mchezo huo kuchangamka.

Mashabiki waliitwa kwa hamasa na wakajaa uwanjani kuishangilia timu ngeni hapa Dar es Salaam na kuwafanya wachezaji wa Singida FG kucheza kwa nguvu .

FUTURE HAWAKUJUA WAFANYE NINI

Kwanza walikuja na akili kuwa Singida FG ni timu ngeni na si timu ya kuwasumbua. Wakaja na mkakati wa kutaka kupata bao mapema kwa mashambulizi ya haraka.

Waliposhindwa kulipata haraka na kuanza kuona ubora wa Singida FG wakataka sasa kucheza kwa kupoteza muda, kujiangusha na kumtaka mwamuzi awasaidie.

SINGIDA FG WALIWEZAJE

Tunajua hii ni timu ngeni kwenye michuano hii na inashiriki kwa mara ya kwanza, hivyo kikubwa walichofanya cha kwanza ni kucheza kwa kujituma na kwa morali kubwa.

Waliingia wakiwa hawana cha kupoteza, Singida FG sio Yanga wala si Simba haina shinikizo ya kulazimika kufanya vizuri, hata kama ingefungwa hakuna mtu wa kuitupia lawama hivyo iliamua kufunguka kuanzia mwanzo mwisho.

WANANE WA SFG

1. Kelvin Kijili:

Zile pumzi na mikimbio aliyoifanya beki wa kulia wa Singida FG huku akirudi kuzuia kwa kasi ileile, hii inamfanya kuwa beki bora wa kulia anayekuja kwa kasi.

Yahya Mbegu:

Kocha Hans Plujm hakuwa hakuwa akimwamini hata kidogo na alikuwa alimpa muda mfupi kucheza, lakini Jumapili kocha mpya amempa nafasi kwenye eneo lake sahihi na hakumuangusha.

Elvis Rupia:

Mshambuliaji mpya ambaye hajacheza mchezo hata mmoja tangu asajiliwe kutoka na sababu tofauti, jana amesimama kuonyesha nini anachotakiwa kukifanya mshambuliaji wa juu, hili ni tatizo kwa kina Meddie Kagere, Thomas Ulimwengu na Francis Kazadi.

Marouf Tchakei:

Mojawapo kati ya usajili bora ambao haujamuangusha aliyemleta, kiungo mshambuliaji bora anajituma na alikuwa tatizo kwa wachezaji wa Future FC.

Aziz Andambwile:

Hakuwa kwenye kiwango bora na alishindwa kabisa kuipandisha timu kutoka nyuma kwenda mbele, ndani ya dakika ya 12, 14, 17 na 23 alipoteza pasi au kunyang’anywa mpira mguuni.

Gadiel Michael:

Alicheza nafasi tofauti na alivyokuwa akicheza kila mara toka akiwa Azam FC, Yanga hadi Simba si beki wa pembeni bali alicheza kama kiungo wa chini.

Labda ndio maana alikuwa bora kwenye kukaba zaidi lakini alikuwa mara kadhaa akipoteza pasi.

Babatunde Bello:

Kiungo wa Future FC ya Misri mwenye asili ya Nigeria ni mchezaji mweusi siyo Mwarabu, ukiona mchezaji wa namna hiyo katikati ya kundi la watu tofauti ujue huyo mtu ana kitu miguuni, ndivyo ilivyokuwa alikaba na kutawanya mipira vizuri

FUTURE IMEFICHA MAKUCHA

Unaweza kujiuliza baada ya kuangalia mchezo kama kweli huo ndio aina ya mchezo ambao uliwafanya Future kuishia hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita.

Jibu ni rahisi tu kuwa kuna muda waliamua kucheza kama kocha wao, Ricardo Formosinho alivyowafundisha, lakini baadaye wakagundua kuwa wapo ugenini kwa hatua hiyo walirudi tena nyuma kuzuia. Naamini bado wana nafasi ya kupindua matokeo ya bao moja hilo na wakapata zaidi ya moja kwenye mchezo wa marudiano utakaofanyika nyumbani kwao Misri.

KWA NINI:

-Ni wepesi wa kufungua na kufika langoni kwa mpinzani kwa pasi za haraka huku wakiifungua timu pinzani kirahisi.

-Wanaweza kujaribu kutumia mfumo huo na hiyo inaweza kuwa silaha ya kupata ushindi nyumbani.

-Hawakufanya makosa mengi langoni mwao.

SINGIDA FG MABADILIKO

Timu imebadilika kiuchezaji huku wachezaji wengi wakicheza kwa kujituma sana . Kuna mabadiliko ndani ya uwanja na zaidi kocha ameanza kumwamini, Mbegu kucheza kushoto ambako alimudu kwa kucheza vizuri sana Ujio wa Elvis Rupia ni ishara tosha kuwa kocha ana jicho la kuona ufanisi wa mchezaji ndani ya uwanja.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live