Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Singida: Ebu wateleni hao Yanga tumalize kazi

Singida Robo Fainali Azam Singida: Ebu wateleni hao Yanga tumalize kazi

Fri, 14 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Singida Big Stars imeweka mikakati ya kuhakikisha inashinda michezo miwili itakayocheza na Yanga katika Uwanja wa Liti huku ikitarajia kuweka kambi jijini hapa kujiandaa na michezo hiyo.

Timu hiyo inasubiria ratiba kujua itacheza lini na Yanga hatua ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na Ligi Kuu Bara.

Michezo hiyo yote inatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Liti mkoani Singida ambapo Singida BS imepata nafasi ya kushiriki hatua ya nusu fainali ya ASFC baada ya kuifunga Mbeya City mabao 4-1 mchezo wa robo fainali uliofanyika uwanja wa Liti.

SBS itacheza mzunguko wa pili wa Ligi Kuu na Yanga mara baada ya mchezo wa mzunguko wa kwanza kukubali kichapo cha mabao 4-1 mchezo uliofanyika Uwanja wa Mkapa, Dar es salaam.

Timu hiyo inashika nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 51, imeshinda michezo 15 na kufungwa mitano.

Msemaji wa timu hiyo, Hussein Massanza alisema wamevunja kambi kwa muda wakisikilizia ratiba kutoka kwa waandaji wa ASFC na Bodi ya Ligi ni lini watacheza michezo yao hiyo dhidi ya Yanga.

“Yanga inafanya vizuri kwahiyo ni mpinzani mgumu lakini tutaenda kupambana nae kwa bahati nzuri mchezo wa nusu fainali umepangwa kuchezwa pale nyumbani hiyo inatupa kujiamini.

“Kambi yetu tutaweka Dodoma tumepapenda Dodoma kutokana na hali ya hewa kufanana na hapa kwetu Singida.

“Mashabiki wasiwe na hofu wala mashaka na ubora wa kikosi chetu tupo katika mfumo, tupo tayari kwa mapambano waje kutusapoti ni michezo muhimu,”alisema Msemaji huyo.

Hata hivyo, Masanza alisema wana furaha kuona malengo waliyojiwekea ya kumaliza katika Top Four na kushiriki mashindano ya kimataifa yametimia kwa asilimia 100.

Chanzo: Mwanaspoti