Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Singida Big Stars yatakata Kaitaba, Mbrazail atupia goli 2

Singida Big Stars Won Kaitaba Singida wameibuka na ushindi wa magoli 2-1

Fri, 21 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mabao mawili ambayo yamefungwa na kiungo mshambuliaji raia wa Brazil, Bruno Gomes yameipa ushindi Singida Big Stars na kuifufua kutoka kwenye kifo baada ya kutopata ushindi kwenye michezo mitatu mfululizo vikiwemo vichapo viwili mbele ya Mtibwa Sugar na Azam FC.

Singida Big Stars imepata ushindi huo ugenini leo saa 10 jioni kwenye Uwania wa Kaitaba mkoani Kagera na kuwapunguza kasi wenyeji Kagera Sugar ambao wameboa kwenye mchezo wao wa kwanza katika uwanja wake wa nyumbani (Kaitaba) baada ya kucheza michezo saba nje ya mkoa huo huku wakipunguzwa kasi ya kushinda mechi mbili zilizopita.

Kagera Sugar ndiyo imekuwa ya kwanza kupata bao la kuongoza likifungwa na mkongwe Hamis Kiiza kwa mtindo wa tik-taka akiunganisha krosi ya Meshack Mwamita baada ya walinzi wa Singida BS kushindwa kuondoa mpira uliotemwa na kipa Metacha Mnata.

Kiiza ameendelea kung'ara ndani ya kikosi hicho ambapo bao alilofunga leo ni la pili mfululizo baada ya wikendi iliyopita kuifungia timu yake bao kwenye matokeo ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ruvu Shooting katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Katika dakika ya 23 kiungo wa Singida, Said Ndemla ameshindwa kuendelea na mchezo baada ya kupata majeraha ambapo nafasi yake imechukuliwa na mshambuliaji, Kelvin Sabatho.

Bao hilo limedumu kwa dakika 45 za kipindi cha kwanza na kuipeleka Kagera Sugar mapumziko ikiwa kifua mbele kwa uongozi wa bao 1-0 huku Singida BS ikirejea kipindi cha pili kwa nguvu mpya na kufanya mashambulizi ya nguvu.

Mnamo dakika ya 51, Singida imepata bao la kusawazisha likifungwa na nyota wa Kibrazil, Bruno Gomes kwa kichwa akiunganisha mpira mrefu uliomiminwa na Paul Godfrey 'Boxer'. Bao hilo limewapa nguvu benchi la ufundi ambalo limemtoa beki wa kati, Biemes Carno na kumuingiza kiungo mshambuliaji, Dario Frederico kuongeza mashambulizi na kusaka mabao ya ushindi.

Dakika ya 63 Kagera Sugar imewapumzisha nyota watatu Ally Ramadhan, Deus Bukenya na Abdallah Seseme kwa mpigo na kuingia Yusuph Mhilu, Yusuph Dunia na Apollinaire Ngueko. Dakika ya 72 ikafanya mabadiliko mengine ikimtoa Hamis Kiiza na kuingia Erick Mwijage.

Singida nao wakajibu mapigo dakika ya 76 ikiwapumzisha Meddie Kagere na Nicholas Gyan na nafasi zao kuchukuliwa na Amissi Tambwe na Frank Zacharia, mabadiliko hayo yamewalipa Walima Alzeti hao mnamo dakika ya 87 wakipata bao la pili likifungwa na Bruno Gomes kufuatia shambulizi la haraka na kufyatua kombora lililojaa nyavuni.

Ushindi huo umewafufua Singida ambao wamefikisha pointi 11 na kupaa hadi nafasi ya sita kutoka ya 10 huku Kagera Sugar wakisalia kwenye nafasi ya 12 na alama zao nane.

Kikosi cha Kagera Sugar: Said Kipao, Datius Peter, Abeid Athuman, Laurent Alfred, Abdallah Mfuko, Deus Bukenya/Yusuph Dunia, Ally Ramadhan/Yusuph Mhilu, Abdallah Seseme/Apollinaire Ngueko, Hamis Kiiza, Mbaraka Yusufu na Meshack Mwamita.

Singida Big Stars: Metacha Mnata, Paul Godfrey 'Boxer', Shafiq Batambuze, Abdulmajid Mangalo, Biemes Carno/Dario Frederico, Aziz Andambwile, Nicolas Gyan/Frank Zakaria, Bruno Gomes, Meddie Kagere/Amissi Tambwe, Said Khamis/Kelvin Sabato na Rodrigo Fegu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live