Uongozi wa Singida Big Stars umetowa hofu Mashabiki wake kwa kusisitiza Mshambuliaji kutoka DR Congo Fancy Kazadi Kasengu ni mali halali ya klabu hiyo, kwa mujibu wa mkataba uliosainiwa mapema mwaka huu.
Kazadi amesajiliwa Singida Big Stars katika kipindi hiki cha Dirisha Dogo la Usajili akitokea Al Masry SC ya Misri, ambako hakuwa na nafasi ya kucheza mara kwa mara tangu aliposajiliwa mwaka 2020.
Uongozi wa Singida Big Stars umetoa taarifa za Mkataba kati yake na Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 30, kufuatia kuibuka kwa tetesi zilizodai Kazadi bado hajasaini mkataba na klabu hiyo, na yupo klabuni hapo kama gelesha.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Singida Big Stars Dismas Ten amesema taarifa zinazosambaa kuhusu Mkataba wa Kazadi na Klabu yao sio za kweli, na kilichopo ni kwamba Mshambuliaji huyo ni mali yao halali.
“Kazadi ni mchezaji wetu halali tena ameshasaini mkataba na Klabu yetu, hizo taarifa sio sahihi kwa sababu zipo tofauti na kilichopo kisheria.”
“Katika hali ya kawaida huwezi kuwazuia watu kusema na kusema kwao kunakuja kwa hali nyingi, ninachokuhakikishia ni kwamba huyu ni mchezaji wetu halali na huko anapotajwa sio sahihi.”
“Watu wanapaswa kufahamu kwamba Singida Big Stars ni Taasisi inayofanya kazi zake kiutaratibu, kwa hiyo hili suala la usajili wa Kazadi lipo kiutaratibu, kwa hiyo ninataka kuweka wazi kuwa tunafanya kazi kwa kufuata weledi na hatubahatishi.” amesema Ten
Kazadi amekua Gumzo katika medani ya Soka la Bongo tangu usiku wa kuamkia leo, kufuatia kufunga mabao manne ya ushindi dhidi ya Azam FC, katika mchezo wa Nusu Fainali ya Kwanza Kombe la Mapinduzi 2023.
Mshambuliaji huyo amefikisha mabao matano kwenye Michuano hiyo, bao lake la kwanza alifunga kwenye mchezo wa Hatua ya Makundi dhidi ya Young Africans uliomalizika kwa sare ya 1-1.