Bao la dakika za 'jioni' lililowekwa kimiani na beki wa kati wa Singida Big Stars, Biemes Carmo jioni ya leo limeiwezesha timu hityo kutinga robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho (ASFC) ikiing'oa JKT Tanzania kwenye mechi kali iliyopigwa Uwanja wa Liti, mjini Singida.
Carmo alifunga dakika ya pili kati ya nne za nyongeza za pambano hilo la hatua ya 16 Bora na kuiwezesha Singida kuzifuata Simba na Geita Gold robo fainali ya michuano hiyo kwa msimu huu.
JKT ambao ndio vinara wa Ligi ya Championship, ilipambana kwa dakika zote za pambano hilo na kuibana Singida na wakati wakiamini kwamba mechi inamalizika kwa sare na pengine kuanza kuwaza mikwaju ya penalti, waliduwaza na mpira wa friikikii uliounganishwa wavuni na kichwa cha Carmo.
Matokeo hayo yameifanya Singida kuungana na Simba iliyoing'oa African Sports kwa mabao 4-0 jana na Geita Gold kuifunga Green Warriors kwa mabao 3-1 katika mechi kali iliyopigwa Uwanja wa Nyankumbu, mjini Geita kutinga robo fainali itakayopangwa wiki ijayo.
Mechi za hatua ya 16 ya ASFC itaendelea tena kesho kwa Mtibwa Sugar kuikaribisha KMC kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani ilihali Ihefu itakuwa wenyeji wa mabingwa wa zamani wa Ligi Kuu Bara, Pan Africans kwenye Uwanja wa Highland Estate, jijini Mbeya.