Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Singida Big Stars wana jambo lao

Singida Fountain Gate Tizi Singida Big Stars wana jambo lao

Sun, 17 Sep 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Achana na matokeo ya mechi za jana za Ligi ya Mabingwa Afrika wakati Simba na Yanga zilipocheza ugenini Zambia na Rwanda, hapa Dar es Salaam leo jioni, Singida Big Stars ina jambo lake kwenye Uwanja wa Azam Complex wakati itakapoikaribisha Future ya Misri katika Kombe la Shirikisho.

Mchezo huo utakaopigwa saa 10:00 jioni unazikutanisha timu hizo, huku Singida ikitinga hatua hiyo kwa kuitoa JKU ya visiwani Zanzibar kwa jumla ya mabao 4-3, ilihali wageni wakianzia raundi ya pili ya michuano hiyo inayoendeshwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Kocha mkuu wa Singida inayoshiriki michuano ya CAF kwa mara ya kwanza, Ernst Middendorp akizungumzia mchezo huo alisema lengo ni kupata matokeo mazuri nyumbani ili kupunguza presha mechi ya ugenini ambayo itakuwa ngumu zaidi kwao tofauti na ya mwanzo.

“Kwa uzoefu wangu hii michezo ya Afrika kila timu inatengeneza mazingira ya kushinda nyumbani, sasa hii ni fursa kwetu ya kutumia vizuri uwanja wetu kisha kujiandaa na marudiano yatakayoamua hatima yetu,” alisema Middendorp, huku beki wa kati wa klabu hiyo, Carno Biemes alisema wao kama wachezaji wako tayari kuipambania timu kwani maandalizi yao yamekamilika na kilichobaki ni kusubiria mchezo husika ili kuwapa raha mashabiki.

“Licha ya kazi kubwa iliyofanywa na benchi letu la ufundi ila sisi wachezaji wenyewe kwa wenyewe tumekuwa pia tukihimizana umuhimu wa mchezo huu na nashukuru kila mmoja wetu ameonyesha utayari wa hilo,” alisema.

Singida inashuka uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya kucharazwa mabao 2-0 katika mechi ya mwisho ya CAF mbele ya JKU baada ya awali kuifunga mabao 4-1, huku ikiwategemea nyota wake kama Joash Onyango, kipa Beno Kakolanya, Bruno Gomes, Meddie Kagere, Francis Kazadi na Marouf Tchakei.

Timu hiyo yenye maskani yake mjini Singida inahitaji ushindi mbele ya Future iliyoanzishwa rasmi mwaka 2011 ikifahamika kama Coca Cola kabla ya Septemba 2, 2021 kubadili jina kuitwa jina la sasa ili kuwa na mazingira mazuri kwa mchezo wa marudiano wiki ijayo utakaopigwa Uwanja wa Al Salam wenye kubeba mashabiki 30,000.

Futureo msimu uliopita timu hiyo ilishinda Kombe la Ligi baada ya ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Ghazl El Mahalla kwenye fainali na kumaliza nafasi ya nne na kufuzu Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya pili mfululizo.

Mshindi wa jumla baina yao atafuzu moja kwa moja hatua ya makundi itakayoanza kuchezwa kuanzia Novemba mwaka huu.

Chanzo: Mwanaspoti