Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Singida Big Stars na bonge la sapraizi

IMG 4271 Singida Big Stars.jpeg Singida Big Stars na bonge la sapraizi

Sun, 11 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ilipanda Ligi Kuu Bara msimu huu kama DTB, lakini hakuna aliyeichukulia kwa uzito mkubwa pengine kwa sababu ilikuwa inayoka Ligi ya Championship.

Fasta mabosi wake wakaibadilisha jina la kuiita Singida Big Stars, lakini ikashtua wadau kutokana na nguvu kubwa iliyokuwa nyuma ya timu hiyo, akiwamo anayetajwa kama mmiliki wake pamoja na safu ya uongozi iliyochagizwa zaidi na aina ya usajili iliyofanya kwa msimu wao wa kwanza.

Ndio, Singida imewasapraizi wengi kwa namna ambayo imeliamsha kwenye Ligi Kuu Bara na Kombe la ASFC ikifika nusu fainali kabla ya kutibuliwa na Yanga ambayo Jumatatu itavaana na Azam iliyoing'oa Simba kwa mabao 2-1.

Pia ni imeingia kwenye orodha ya timu zilizowahi kupanda daraja na kuvuna pointi nyingine, kwani kabla ya mechi za jana za kufungia msimu, Singida ilikuwa na pointi 54 kutokana na mechi 29.

KMC iliwahi kumaliza msimu na pointi kama hizo lakini katika mechi 38, wakati Namungo ilivuna pointi 64 ikiwa ni rekodi iliyopo kwa sasa kwa timu iliyopanda daraja la kukusanya pointi nyingi, lakini ni kwa kupitia mechi 38, tofauti na ilivyo kwa Singida. Mechi chache pointi nyingi.

KIKOSI CHA KIBABE

Singida iliyopo chini ya jopo la makocha wa kimataifa watatu wakiongozwa na Hans Pluijm, Ramadhani Mswazurwimo na Mathias Lule ni moja ya timu yenye kikosi chenye mastaa kutoka nchi mbalimbali wakiwamo wazawa na wageni.

ndio klabu iliyokuwa na idadi kubwa ya wachezaji kutoka Brazili, pia ilikuwa na Muargentina, Wakongoman, Wa Ivory Coastal, Ghana, Uganda, Rwanda, Burundi mbali na Watanzania wenye majina makubwa kwenye soka la Tanzania na Afrika Mashariki na Kati kwa ujumla.

Utatu wa Deus Kaseke, Bruno Gomes na Meddie Kagere na kwa mbaalii, Amissi Tambwe imeifanya Singida kuwa tishio kwa msimu wa kwanza wa ushiriki wa ligi hiyo.

Bruno ambaye ni Mbrazili ndiye kinara wa mabao wa timu hiyo (kabla ya mechi za jana) akiwa na mabao 10, akifuatiwa na Meddie Kagere mwenye mabao nane na kuiwezesha timu hiyo kuwa na mabao 34, ikiwa inashika nafasi ya nne sambamba na Geita Gold na Mbeya City, nyuma ya Simba yenye mabao 72, Yanga (59) na Azam (47).

Katika dirisha dogo iliongeza mashine nyingine ambazo baadhi yao imeifanya iwe imara zaidi na pengine kwa msimu ujao mambo yatakuwa moto zaidi iwapo hakutakuwa na mabadiliko makubwa.

USHINDI MWINGI

Singida ni kati ya timu nne zilizopata ushindi mwingi, ikitanguliwa na Yanga iliyoshinda mechi 24, Simba (21) na Azam iliyoshinda mechi 17, ikiwa ni moja zaidi na ilizoshinda Singida kwa kila timu ikicheza mechi 29 (kabla ya za jana za kufungia msimu).

Singida pia ni moja ya timu zilizopata matokeo mazuri kwenye uwanja wa nyumbani kwani katika mechi 15 imeshinda 11 kutoka sare ya mbili na kupoteza mbili, ikishika nafasi ya tatu nyuma ya Yanga iliyocheza mechi 15 na kushinda 13 na kutoka sare mbili huku ikiwa haijapoteza, huku Simba ikiwa ya pili kwa kucheza mechi 14 (kabla ya jana) ikishinda 12 na kudroo mbili pia bila kupoteza kama watani wao.

Katika mechi za nyumbani Singida imevuna jumla ya pointi 35, na mabao 21 ya kufungwa na kufungwa manane tu, ikiwa ni kati ya timu tatu zilizoruhusu mabao machache nyumbani ikitanguliwa na Yanga (mabao 7) na ikilingana na Simba iliyofungwa pia manane.

Kwa mechi za ugenini (kabla ya jana) Singida ilikuwa ikishika nafasi ya nne, nyuma ya Yanga ambayo iliyocheza 14 na kushinda 11, ikitoka droo moja na kupoteza moja (kabla ya mechi yao ya jana dhidi ya Tanzania Prisons)

Simba inashika nafasi ya pili kwa kucheza mechi 15 ikishinda tisa, ikitoka sare tano na kupoteza moja, huku Azam ikifuatia kwa kucheza mechi 15 ikishinda sita, sare nne na kupioteza tano kisha ndipo Singida inafuata ikicheza michezo 14, ikishinda mitano, sare nnne na kupioteza mitano pia.

Timu hiyo kwa mechi za ugenini imevuna pointi 19 mabao 13 ya kufungwa na kufungwa 17 ikiwa ni timu inayoshika nafasi ya tatu ya kufungwa mabao machache ugenini baada ya Siomba (8), Yanga (11), ikilingana na Azam na Namungo.

MAMBO NI MOTO

Katika kuonyesha kwamba Singida imepania kufanya kweli kwenye soka la Tanzania, tayari imeanza mipango ya msimu ujao kwa kusajili kimya kimya majina makubwa kwenye kikosi chao, licha ya baadhi ya nyota wake kutajwa kuhitajiwa na vigogo Simba, Yanga akiwamo Bruno.

Tayari kuna majina makubwa yanayotajwa kupewa mikataba ya awali na Singida akiwamo kipa Beno Kakolanya aliyepo Simba, huku majina mengine yakifanywa siri na Kocha Hans Pluijm alikaririwa kwamba wanataka kutengeneza kikosi kazi kwa msimu ujao wa michuano ya CAF.

"Kiu yetu ni kumaliza kwanza nafasi ya tatu (kabla ya jana kushuka uwanjani), ili kuwapiku Azam waliopo juu yetu, lakini tuna malengo makubwa kwa msimu ujao ikizingatiwa tayari tuna tiketi ya michuano ya CAF," alikaririwa Hans Pluijm.

Kocha huyo raia wa Uholanzi, alisema usajili wao utawekwa bayana na unafanywa kwa kuzintaia mahitaji ya timu kwa vile kikosi cha sasa kimejitosheleza, licha ya kuwepo na maeneo yenye kuhitaji kuboreshwa zaidi ili timu iwe imara zaidi ligi za ndani na kimataifa.

Ofisa Habari wa timu hiyo, Hussein Massanza naye alikaririwa mapema kwamba, kuna wachezaji watakaosajiliwa Singida kwa lengo la kuimarisha kikosi, huku akiweka bayana mipango yao ya kuwa na timu ya soka ya wanawake kama moja na sharti la ushiriki wa michuano ya CAF msimu ujao.

Singida itashiriki Kombe la Shirikisho sambamba na Azam FC ambazo ni kati ya timu zisizokuwa na timu za wanawake, hivyo kulazimika kuzianzisha na kutuma taarifa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kabla ya Juni 30 mwaka huu.

Massanza alisema hawana hofu na agizo hilo la CAF, kwani mipango ilikuwa ikifanywa wakati timu hiyo ikimalizana na Namungo kwenye mchezo wa mwisho wa kufungia msimu ikiwa ugenini mjini Ruangwa Lindi.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: