Ushindi wa mabao 3-0 iliyopata juzi dhidi ya Polisi Tanzania kwenye uwanja wa nyumbani wa Liti, mjini Singida umeifanya Singida Big Stars izidi kujikita nafasi ya tatu katika Ligi Kuu Bara na kuinusa tiketi ya CAF.
Polisi inayoshika mkia kwenye msimamo wa ligi hiyo, ilizidi kujiweka pabaya kwa kipigo hicho kilichotokana na mabao mawili ya mabeki, Pascal Wawa na Nickson Kibabage waliofunga dakika ya 13 na 57, kisha mkongwe Amissi Tambwe akatupia la tatu dakika ya 90 akitokea benchi.
Licha ya kupoteza mchezo, Polisi inayonolewa na Mwinyi Zahera ilijitutumua kutaka kurudisha mabao hayo, lakini ilizidiwa akili na mabeki wa Singida.
Matokeo hayo yameifanya Singida kufikisha pointi 51 baada ya mechi 26 ikijiweka pazuri kunasa tiketi ya michuano ya CAF msimu ujao, huku Polisi ikisalia mkiani na alama 19 wakati ligi imebaki mechi za nne kabla haijamalizika.