Mchezo wa robo fainali ya mashindano ya Azam Sports Federation (ASFC) kati ya Singida Big Stars dhidi ya Mbeya City umelizika katika uwanja wa Liti mkoani Singida kwa wenyeji kuibuka na ushindi wa mabao 4-1
Ilikuwa siku nzuri kazini kwa kiungo fundi Bruno Gomes ambaye katika mchezo huu amefunga mabao mawili dakika za 7 na 57 huku mabao mengine yakifungwa na Bright Adjei na Francy Kazadi katika dakika za 10 na 27.
Bao la kufutia machozi la Mbeya City lilifungwa na mshabuliaji Eliud Ambokile dakika ya 55 ambaye aliingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Juma Shemvuni.
SBS itasubiri mshindi kati ya Yanga na Geita ambazo zinatarajiwa kucheza Aprili 8 mwaka huu katika uwanja wa Azam Complex Chamanzi Jijini Dar es salaam.
Mchezo wa nusu fainali kati ya SBS na mshindi kati ya Yanga na Geita Gold unatarajiwa kupigwa katika uwanja wa Liti mkoani Singida.
ZIFUATAZO NI DONDOO MUHIMU ZA MCHEZO HUU
Mbeya City haijawahi kupata ushindi katika michezo miwili iliyokutana kwenye ligi na SBS,mchezo wa mzunguko wa kwanza uwanja wa Liti Mbeya City ilichapwa mabao 2-1 na mchezo wa pili zikatoka sare ya bao 1-1 uwanja wa Sokoine Mbeya.
Katika mchezo huu,mwamuzi Ramadhan Kayoko kutokea Dar es salaam alitoa kadi moja ya njano aliyomuonesha Aziz Andambwile wa SBS kutokana na kumchezea faulo Richardson Ng'odya. Singida Big Stars tayari imejihakikishia kucheza kombe la Shirikisho barani Afrika msimu ujao kwa kumaliza kwenye ‘top Four’ katika msimamo wa ligi Kuu Bara.
Katika mchezo huu winga wa SBS Nickson Kibabage ametengeneza mabao mawili (Assist) kwa wachezaji Francy Kazadi na Bright Adjei kwenye dakika za 10 na 27.
Winga wa Mbeya City,Richardson Ng’odya anashika nafasi ya tatu kwa ufungaji akiwa na mabao matano huku Andrew Simchimbi wa Ihefu akiongoza akiwa na mabao saba akifuatiwa na Clement Mzize wa Yanga mwenye mabao sita.
Kocha wa SBS aliwatoa Bruno Gomes,Nickson Kibabage,Bright Adjei, Paschal Wawa na Francy Kazadi na nafasi zao zilichukuliwa na Deus Kaseke,Nasoro Saadun, Amiss Tambwe,Hamad Waziri na Rodrigue Tegu. Kwa upande wake Kocha wa Mbeya City,Mubiru Abdallah aliwaingiza Hassan Machezo,Eliud Ambokile na George Sangija na kuwatoa Awadh Juma, Baraka Mwalubunju na Juma Shemvuni.
Mbeya City hiyo ndio mara yake ya kwanza kutinga hatua ya robo fainali tangu ilipopanda daraja msimu wa 2013-2014 mara zote imekuwa ikiondolewa hatua za awali.
Mapema dakika ya 6 beki wa Mbeya City,Samson Madeleka aliumia na kukimbizwa Hospitali wakati akimdhibiti Kibabage asilete madhara na nafasi yake ilichukuliwa na Hassan Mohammed.