Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Singida BS yavuruga usajili Simba, yavamia Ivory Coast

Usajiliiiii Singida BS yavuruga usajili Simba, yavamia Ivory Coast

Mon, 24 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Singida Black Stars (zamani Ihefu), imeendelea kusuka kikosi kwa ajili ya msimu ujao ikielezwa imepora nyota wawili wa kigeni waliokuwa wakihusishwa na Simba, huku ikimalizana na makipa Metacha Mnata na Beno Kakolanya ambaye anaweza akapelekwa kwa mkopo Namungo.

Singida iliyobadilishwa jina hivi karibuni na kuhamishia maskani mjini Singida kutoka Mbarali ilikokuwa wakati ikitumia jina la Ihefu, inadaiwa tayari imewasainisha mikataba wachezaji wawili kutoka ASEC Mimosas ya Ivory Coast, beki Anthony Tra Bi Tra na kiungo Serge Pokou, waliokuwa wakiwindwa na Simba.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya klabu hiyo imelithibitishia Mwanaspoti kuwa, nyota hao kila mmoja amesaini mkataba wa miaka miwili na tayari wamelipwa kiasi cha fedha za dau la usajili na wamepewa ratiba ya kujiunga kambini kujiandaa na msimu mpya wa mashindano kwa mwaka wa 2024-2025.

Ukiachana na wachezaji hao wa kigeni, jina lingine linalotajwa ni kiungo mkabaji Zawadi Mauya anayedaiwa amesainishwa pia mkataba wa miaka miwili baada ya kumaliza mkataba na Yanga aliyokuwa akiichezea tangu alipojiunga nayo Julai, 2020 akitokea Kagera Sugar.

“Wachezaji kutoka ASEC Mimosas wameishatumiwa barua ya lini wanatakiwa kuingia kambini kwa ajili ya kujiunga na wenzao kwa maandalizi ya msimu mpya na pesa zao za usajili wamepewa kiasi hawajamaliziwa zote,” kilisema chanzo hicho na kuongeza; “Bado tunaendelea na usajili, kwani tayari kuna wachezaji wa ndani ambao wamesajiliwa kama Kakolanya, Metacha, Mauya na wengine ambao tupo kwenye mazungumzo nao.”

Mkurugenzi wa Utawala wa timu hiyo, Muhibu Kanu alipotafutwa na Mwanaspoti ili kuthibitisha taarifa hizo, alishindwa kukubali au kukataa kwa kuishia kusema; “Tayari kocha ametoa ripoti, ila sijaisoma ina wachezaji gani, huenda wapo ama la, hivyo ni vizuri ungenitafuta kesho (leo) Jumatatu jioni naweza kuwa majibu.”

Licha ya kutotaja wachezaji wengine wazawa waliotua Singida BS, Mwanaspoti linafahamu kuwa beki Yahya Mbegu aliyekuwa Singida FG naye ameshamalizana na klabu hiyo na msimu ujao ataichezea timu hiyo.

Chanzo: Mwanaspoti