Uongozi wa Singida Big Stars umeachana na aliyekuwa Ofisa Mtendaji wake Mkuu, Dismas Ten baada ya kufikiwa maamuzi hayo na viongozi.
Ten aliyekuwa Ofisa Habari wa Yanga na Mbeya City aliteuliwa rasmi kuchukua cheo hicho Julai 26 mwaka jana, akichukua nafasi ya Muhibu Kanu aliyehamishiwa kitengo cha Mkurugenzi wa Masoko na Fedha na kuiwezesha kupata wadhamini wengi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ibrahim Mirambo, alithibitisha taarifa hizo huku akieleza ni jambo la kawaida kwenye taasisi kwani kabla ya uteuzi wake tayari kulikuwa na mtu mwingine aliyekuwa anaendelea na majukumu.
"Ten tumempangia majukumu mengine ingawa siyo vyema kuyaeleza hapa, bado atabaki hapa ila ni kwenye nafasi nyingine tofauti na aliyokuwa nayo hapo mwanzo, mabadiliko haya hayawezi kutuathiri hivyo mashabiki waendelee kutupa sapoti yao."
Mirambo aliongeza baada ya kuondoka kwa Ten kwenye cheo hicho kwa sasa ambaye amepewa jukumu hilo ni, John Kadutu ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa ni Mkurugenzi wa utawala huku akishirikiana kwa ukaribu katika majukumu hayo na Muhibu Kanu ambaye aliondolewa hapo awali.