Uongozi wa Klabu ya Singida Big Stars umechimba mkwara kuelekea mchezo wa Mzunguuko wa 27 wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambao utawakutanisha na Mabingwa watetezi Young Africans mwezi Mei kwenye Uwanja wa Liti mjini Singida.
Singida ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikiwa imebakiza michezo minne kukamilisha msimu huu jambo ambalo wameahidi kufia uwanjani.
Meneja wa Singida Big Stars, Ibrahim Mohammed amesema, wanatafuta nafasi ya kujihakikishia kushiriki michuano ya kimataifa, hivyo wamejipanga kupata ushindi kwenye michezo yote minne iliyosalia.
“Lengo letu kwa sasa ni kumaliza katika nafasi ya tatu ili tupate nafasi ya kushiriki kimataifa msimu ujao, hivyo tayari sisi kama uongozi tumeshazungumza na wachezaji na wameahidi kufanya hivyo.
Njia pekee ya kuhakikisha tunatimiza hilo ni kupata ushindi kwenye michezo yetu yote iliyosalia, hivyo hatutarajii kuiona timu ikija hapa Singida na kutoka na ushindi dhidi yetu,” amesema.
Young Africans itakwenda Singida ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza mchezo wa Mzunguuko wa 26 Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Simba SC kwa kufungwa 2-0, Juzi Jumapili (April 16).
Hata hivyo kabla ya kuelekea mjini Singida, Young Africans itacheza mchezo wa Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Rivers United ya Nigeria.
Mchezo wa mkondo wa kwanza utashuhudia Young Africans ikicheza ugenini Nigeria April 23, kasha itarejea jijini Dar es salaam kukipiga katika Uwanja wa Benjamin Mkapa April 30.