Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Singida BS: Tunamtaka Chama, Tchakei haondoki

Chama Clatous Name Clatous Chama

Fri, 3 May 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Uongozi wa Singida Black Stars (Ihefu SC) umesema Clatous Chama ni mchezaji unayetamani kuwa naye msimu ujao, ukibainisha kuwa iwapo muda utafika kila kitu kitakuwa wazi kwa kuwa bado staa huyo ana mkataba na Simba.

Pia umesisitiza kuwa hautakuwa tayari kumuachia mchezaji ambaye yupo kwenye mipango ya timu hiyo hasa Mtogo Marouf Tchakei ambaye anazitoa udenda timu kubwa hapa nchini.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mkurugenzi wa Utawala wa timu hiyo, Muhibu Kanu amesema ishu ya kumtaka Chama ni mapema kuizungumzia, lakini ni miongoni mwa wachezaji wanaowatamani kuwa nao kikosini.

Amesema kwa sasa wanaheshimu mkataba alionao katika timu yake, hivyo muda ukifika wakakubaliwa ofa yao hawatasita kumvuta kwani malengo ya Singida Big Stars ni kucheza kimataifa msimu ujao.

Chama anadaiwa kwamba yupo katika siku zake za mwishomwisho Msimbazi kulingana na mkataba wake, na kwa sasa amefungiwa mechi tatu na Bodi ya Ligi kutokana na kumkanyaga kwa makusudi Nickson Kibabage wa Yanga katika mchezo wa Dabi ya Kariakoo, wiki chache zilizopita.

“Chama hakuna asiyemfahamu uwezo wake na sisi Singida BS tunatamani kuwa naye japokuwa kwa sasa tunaheshimu mkataba wake na hatutaki kulizungumza sana. Tusubiri akikubali ofa yetu tutaweka wazi,” amesema Kanu.

Kigogo huyo ameongeza kuwa zipo tetesi za baadhi ya timu zikiwamo kongwe nchini zinazommendea Tchakei na kwamba ni furaha wachezaji wao kutajwa na timu kubwa, lakini kamwe hawamuachii.

“Sisi hatutakubali kuruhusu wachezaji wetu walio kwenye mipango kuondoka, lakini wengine tunaweza kuruhusu kama watatoa dau kubwa tukafanya biashara,” amesema bosi huyo.

Kuhusu mwenendo wa timu hiyo, kiongozi ambaye ni kocha kitaaluma amesema kwa sasa yapo mabadiliko na mkakati wao ni kutinga fainali Kombe la Shirikisho Bara (FA) na pia kumaliza ndani ya nafasi nne za juu kwenye Ligi Kuu.

“Kwenye Ligi Kuu bado tuko nyuma kimalengo, lakini hatujakata tamaa na matarajio yetu ni kumaliza nne bora. Wakati huohuo tunaitaka fainali ya Kombe la Shirikisho na hatuogopi yeyote,” amesema kiongozi huyo.

Singida Black Stars awali ilijulikana Ihefu ambayo makazi yake yalikuwa wilayani Mbarali mkoani Mbeya kabla ya kuihamishia mkoani Singida ambapo baada ya kufuzu nusu fainali shirikisho, itakutana na Yanga kutafuta kutinga fainali.

Chanzo: Mwanaspoti