Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simu zao zitaita Ten Hag atakapofukuzwa Man United

Zidane 1 Simu zao zitaita Ten Hag atakapofukuzwa Man United

Wed, 17 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kibarua cha Erik ten Hag huko Manchester United kimejaa mashaka matupu kwa sasa. Miamba hiyo imetupwa nje ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na Kombe la Ligi, hali ya maisha si nzuri kwenye Ligi Kuu England, kibarua kinawezaje kuwa salama?

Kutokana na hilo, tayari kuna orodha ya makocha kadhaa wameanza kuhusishwa na miamba hiyo ya Old Trafford, huenda simu zao zikaita, kuulizwa kama watakuwa tayari kwenda kufanya kazi kwenye timu hiyo.

Kwa mujibu wa Oddscheker hii hapa orodha ya makocha ambao wanaweza kwenda kupewa mikoba ya kuinoa Man United wakati Mdachi Ten Hag atakapopigwa kibuti na kuonyeshwa mlango wa kutokea huko Old Trafford. Nani atakubali? Graham Potter

Hebu vuta hisia, Man United inamfuta kazi Ten Hag na kisha inampa timu Graham Potter, mtu ambaye alifeli alipokuwa kwenye timu nyingine ya Big Six, Chelsea.

Ni kama haingii akilini hivi, lakini ukweli kocha huyo wa zamani wa Brighton ni moja ya makocha wanaopendwa na bosi mpya wa Man United, Sir Jim Ratcliffe – hivyo chochote kinaweza kutokea.

Potter alifanya kazi nzuri sana alipokuwa Brighton, lakini mambo yaligoma alipokuwa Chelsea na Man United haiwezi kuliona hilo kama kikwazo cha kushindwa kumpa timu kocha huyo ili kuja kuonyesha ubabe wake Old Trafford.

Julen Lopetegui Ni mtu mwenye uzoefu wa kuzifundisha timu za klabu na timu za taifa. Aliwahi kuinoa timu kubwa Ulaya kama Real Madrid, hivyo anafahamu wazi presha za kuwa kocha kwenye timu za aina hiyo. Kwenye Ligi Kuu England aliwahi kuinoa Wolves, hivyo anafahamu vyema pia mikikimikiki ya kwenye ligi hiyo.

Man United inaweza kwenda na chaguo la kumnasa Mhispaniola huyo ili kwenda kuweka vionjo vya soka la Kihispaniola kwenye kikosi chao na huenda ukahamishia masuala ya usajili kwa nchi ya Hispania baada ya sasa kocha Ten Hag kuwa bize kuleta wachezaji waliotamba Uholanzi.

Ruben Amorim Jina la Zinedine Zidane na la kocha wa Sporting, Ruben Amorim ni miongoni mwa yaliyokuwa yakihusishwa na miamba ya Old Trafford kwamba watakwenda kuinoa Manchester United.

Mwanzoni ilionekana kama habari hiyo haina ukweli wowote, lakini kinachoelezwa kwa sasa, kocha huyo mwenye umri wa miaka 38 ni miongoni mwa watu wanaopewa nafasi ya kwenda kufanya kazi ya kuinoa Man United.

Hakuna shaka kwamba kocha Amorim atakuwa ni kitu anachokisubiri kwa hamu kuona kinatokea kwa maana ya kupigiwa simu akainoe Man United wakati Ten Hag atakapotupwa nje.

Roberto De Zerbi Hakuna ubishi ni aina ya kocha ambaye atakubalika kwa asilimia zote na mashabiki wa Manchester United kutokana na namna alivyoifanya Brighton kuwa timu bora zaidi ndani ya uwanja katika kipindi cha miezi 12 iliyopita.

Lakini, kinachowatisha kiasi Man United ni kuhusu kile ambacho alikwenda kukifanya Potter huko Chelsea baada ya kutokea Brighton. Kinachoonekana Brighton ni mfumo wa kiuchezaji na si uwezo wa mtu mmoja mmoja.

Lakini, De Zerbi ni mmoja wa makocha wenye vipaji ambao hakuna timu itagoma kuwa nao kwenye vikosi vyao kwa soka la kisasa.

Hansi Flick Flick bado anauguza maumivu ya kufutwa kazi kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Ujerumani, Septemba mwaka jana baada ya kuiongoza timu hiyo kwenye ushindi wa mechi 12 kati ya 25, tangu aliporithi mikoba kutoka kwa Joachim Low mwaka 2021.

Lakini, alipokuwa Bayern Munich, rekodi zake zilikuwa tamu sana na alishinda mechi 70 kati ya 86 na alipafanya Allianz Arena kuwa mahali tishio.

Katika miezi yake 18 aliongoza Bayern kushinda mataji matatu msimu wa 2019/20. Kocha Flick halitakuwa chaguo baya kama atanaswa na Man United kwenda kuchukua mikoba ya Ten Hag atakapoondoka.

Andoni Iraola Kikosi chake cha Bournemouth kilishinda mabao 3-0 uwanjani Old Trafford ili kupigilia msumari kabisa anafaa kupewa mikoba ya kuinoa Man United kwa sababu alimtesa Ten Hag akiwa na wachezaji wa kawaida tu.

Akiwa na umri wa miaka 41, Iraola ni kocha kijana mwenye ufahamu mwingi wa soka la kisasa, ambaye ataweza pia kumudu presha za kuwa kocha kwenye timu kubwa na inayohitaji ushindi katika kila mechi kama ilivyo Man United. Haitakuwa kitu cha kushangaza kama litasikika jina la Iraola kwenye wale wanaohusishwa na kibarua cha kwenda kuinoa miamba hiyo ya Old Trafford.

Zinedine Zidane Kocha huyo wa zamani wa Real Madrid amekuwa hana kazi kwa zaidi ya miaka miwili na sasa anahitaji kurudi mzigoni. Mwenyewe aliwahi kusema amepumzika kwa kiasi cha kutosha sasa yupo tayari kwa ajili ya kurudi kwenye kazi hiyo yenye presha nyingi.

Huko nyuma Man United ilishawahi kuhusishwa na mpango wa kumchukua Zidane, kabla ya dili hilo kushindwa kukamilika. Siku karibuni, alitajwatajwa na kuhusishwa na PSG, lakini Mfaransa huyo bado hana kazi na Man United itakuwa imefanya chaguo sahihi ikimwajiri. Zidane ni mwamba wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kieran McKenna Kwa sasa yupo kwenye mbio za kuhangaika kuipandisha Ipswich Town huko kwenye Championship. Anatajwa kwenye orodha hii kwasababu ni kocha mwenye uelewa wa utamaduni wa Man United kutokana na kuwahi kuwa na timu hiyo kwa muda mrefu.

McKenna anawekwa kwenye kundi moja na Michael Carrick wanaifahamu historia ya miamba hiyo ya Old Trafford, wawili hao wanaweza kuwa kwenye orodha ya wanaoweza kupewa kibarua cha kuonoa Man United wakati Mdachi Ten Hag atakapoonyeshwa mlango wa kutokea. Kuhusu McKenna jina lake litashangaza wengi likitajwa Old Trafford.

Ralph Hasenhuttl Si jina ambalo mashabiki wa Man United watavutiwa nalo hasa wakiangalia rekodi zake kwenye kikosi cha Southampton, kwamba kwa namna moja au nyingine alihusika kwenye kuishusha daraja timu hiyo.

Hata hivyo, Man United ni mahali ambako kocha unapewa sapoti ya kutosha unapohitaji wachezaji wa kuja kuongeza ubora kwenye kikosi chake, hivyo jambo hilo linaweza kumfanya Hasenhuttl kwenda kufanya kweli Old Trafford.

Kuna miamba ambayo kocha huyo alifanya mambo makubwa huko St Mary’s na kuhusishwa na Man United, hivyo si jina tu lililoibuka tu kutoka kusikojulikana.

Antonio Conte Kwenye Ligi Kuu England, Mtaliano Antonio Conte amepata umaarufu baada ya kuinoa Chelsea na kunyakua ubingwa wa ligi hiyo katika msimu wake wa kwanza tu. Aliwahi kuinoa pia Tottenham Hotspur, hivyo anafahamu nje ndani ugumu wa Ligi Kuu England na presha ya kuwa kwenye timu zinazojiita Big Six.

Kuhusu uzoefu wa kuzinoa klabu kubwa, Conte kwenye hilo amefaulu vyema, akiwahi kuzinoa pia Juventus na Inter Milan, ambayo ni miamba ya soka ya huko Italia. Kwa kipindi hiki, jina lake limekuwa likihusishwa na timu za AS Roma na AC Milan, zinataka huduma yake akapige kazi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live