Kocha wa Atletico Madrid, Diego Simeone atakuwa katika presha kubwa leo wakati timu yake itakapokuwa ugenini kuvaana na Porto katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Msimamo wa kundi lao B ulivyo, unawalazimisha Simeone na vijana wake kuhakikisha wanashinda mechi hiyo ya ugenini ili wajihakikishie kutinga hatua ya 16 bora ya mashindano hayo.
Matokeo ya ushindi yataifanya Atletico Madrid kufikisha jumla ya pointi saba ambazo zinaweza kuwafanya wamalize katika nafasi ya pili lakini hilo nalo litategemea matokeo ya mchezo baina ya AC Milan na Liverpool ambayo tayari imeshafuzu kwa kujihakikishia uongozi wa kundi hilo.
AC Milan kama itaifunga Atletico Madrid, inaweza kusonga mbele hata kama Atletico Madrid itashinda dhidi ya Porto kwani zitamaliza zikiwa na pointi sawa na hivyo yenyewe inaweza kunufaika na utofauti mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa ikiwa itafanikiwa kupachika mabao mengi leo.
Na ikiwa Atletico itapoteza mchezo huo na kushika mkia wa kundi hilo, ni wazi kwamba litakuwa ni pigo kubwa kwa timu hiyo na Simeone kwa ujumla katika mashindano ya Ulaya na itakuwa mara ya pili kwao ndani ya kipindi cha misimu 10 baada ya kuishia katika hatua hiyo msimu wa 2017/2018.
Lakini kwa Porto walio nafasi ya pili katika kundi hilo wakiwa na pointi tano, wanahitaji ushindi tu leo ili waweze kutinga hatua inayofuata.
Na kingine kinachoongeza ugumu zaidi kwa Simeone katika mchezo huo ni kukosekana kwa nyota wake muhimu ambao wanakabiliwa na majeruhi nao ni Stefan Savic, Kieran Trippier, Ivan Saponjic na Jose Gimenez.
Atletico Madrid imekuwa haina mwenendo wa kuridhisha katika siku za hivi karibuni jambo linalomuweka Simeone katika wakati mgumu ambapo imepata ushindi mara tatu tu kwenye mechi 10 ilizocheza za mashindano yote.