Mabao mawili aliyofunga Simchimba yanamfanya kuendelea kubaki kileleni kwenye orodha ya ufungaji bora kwenye michuano ya kombe la shirikisho kwa kufikisha saba akimuacha moja Mzize wa Yanga.
Wakati jana kinda wa Yanga, Clement Mzize akiisaidia timu yake kufuzu robo fainali ya kombe la shirikisho (ASFC) huku akikaa usukani kwa muda kwa idadi ya mabao sita, leo straika wa Ihefu Andrew Simchimba amejibu mapigo na kumshusha kileleni.
Yanga ikicheza jana kwenye uwanja wa Azam Complex iliiburuza Tanzania Prisons mabao 4-1 na kutinga nane bora ya michuano hiyo, huku Mzize akifunga mabao mawili na kufikisha sita kwenye akaunti yake.
Kabla ya mchezo huo, Mzize aliyepandishwa msimu huu alikuwa ametoka kufunga mabao manne wakati Yanga ikitakata mbele ya Kurugenzi FC kwa mabao 8-0 huku mengine yakifungwa na Yusuph Athuman (mawili) moja wakijifunga na David Bryson.
Idadi hiyo ilimfanya kumshusha Simchimba aliyekuwa na matano aliyofunga kwenye mechi moja wakati Ihefu ikiilima Mtama Boys ya mkoani Mtwara mabao 9-0 na leo tena nyota huyo ameendelea kutupia.
Ihefu ikicheza katika uwanja wake wa nyumbani Highland Estate mkoani Mbeya imeilalua Pan Africa ya Championship mabao 2-0 na yote yakiwekwa wavuni na straika huyo akianza kwa penalti dakika 36 kisha dakika ya 50 akimalizia pasi ya Yacouba Sogne.
Mbali na kukaa kileleni lakini ushindi huo umeipa faida Ihefu kuungana na Simba, Yanga, Singida BS na Geita Gold zilizotangulia mapema kwenye nane bora ya michuano hiyo.
Hata hivyo Straika huyo aliyeipandisha timu hiyo ligi kuu kabla ya kushuka na kurejea nayo tena ameshindwa kumaliza dakika 90 baada ya kuumia na kutolewa nje.