Baada ya kutwaa medali ya shaba jana asubuhi na kufuzu kushiriki mashindano ya dunia mwaka huu na michezo ya Olimpiki 2024, nyota wa mbio ndefu za barabarani nchini, Alphonce Simbu ameanza kuweka mikakati ya medali za mashindano hayo.
Simbu aliyetumia saa 2:06:19 alimaliza wa tatu mbio ya Osaka marathoni nchini Japan, akiachwa kwa sekunde 18 na bingwa raia wa Ethiopia, Hailemaryam Kiros aliyetumua saa 2:06:01 na Mkenya, Victor Kiplagat aliyetumia saa 2:06:03 alimaliza wa pili.
Akizungumzia ushindani wa mbio hiyo jana, Simbu alisema wapinzani wake walimpita wakiwa wamebakiza kilomita mbili kusika eneo la kumalizia mbio.
"Nilikwenda nao sambamba, kuna muda nilikuwa naongoza na wao wanaongoza, tulikwenda sambamba muda mrefu hadi tukiwa kilomita ya 40 wakaniacha kidogo," alisema nyota huyo ambaye mbali na medali ya fedha, amevunja muda wake kwa sekunde moja.
Kwa matokeo hayo, Simbu sasa amefuzu kuiwakilisha nchi kwenye mashindano ya dunia ya Agosti huko Budapest, Hungary na michezo ya Olimpiki ya 2024, Paris Ufaransa.
"Naanza safari ya kurudi nyumbani kesho (leo) keshokutwa (kesho) nitakuwa huko kwa ajili ya kuanza maandalizi ya mashindano hayo, nitaanza na yale ya dunia kwanza, lengo ni kuhakikisha najiandaa mapema ili niweze kufanya vizuri," alisema Simbu ambaye atawasili saa 7 mchana kwenye uwanja wa ndege wa Dar es Salaam kabla ya saa 10 jioni kubadili ndege kwenda Arusha.
Simbu miongoni mwa nyota watano walio kwenye ufadhili wa Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC) kupitia kitengo chake cha misaada (Olympic Solidarity) anakuwa Mtanzania wa kwanza kufuzu Olimpiki ijayo.
Rekodi bora ya Simbu kwenye mashindano kama hayo ni ile ya 2019 aliposhinda medali ya shaba ya dunia na kwenye Olimpiki ya Rio 2016 alimaliza wa tano kwenye marathoni. Kocha wa nyota huyo, Francis John alisema muda aliokimbia
Simbu nchini Japan umemuwezesha kufikia viwango vya vya Shirikisho la Riadha la Dunia (WA) kwa ajili ya Olimpiki ijayo na mashindano ya dunia ambako ili ufuzu unapaswa kukimbia kwa saa 2:08:10 na 2:09:40.
"Mipango yangu ya awali imetiki, nilitaka afuzu mbio za dunia na Olimpiki, amefikia kote, sasa tunaanza kujipanga kwa ajili ya mashindano hayo, ataendelea kujifua na kushiriki mashindano mbalimbali ya kimataifa ili kuboresha muda wake," alisema kocha Francis.