Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simbu, Geay wakosa medali, Tola akishinda kwa rekodi

Olympic Paris Tz Simbu, Geay wakosa medali, Tola akishinda kwa rekodi

Sat, 10 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Wanariadha Alphonce Simbu na Gabriel Geay wameshindwa kufurukuta katika mbio za Marathoni (Wanaume) katika Michezo ya Olimpiki inayoendelea, Paris Ufaransa huku Tamirati Tola wa Ethiopia akiibuka mshindi leo Jumamosi akiwema rekodi mpya wa michezo hiyo.

Tola (32) aliibuka mshindi wa kwanza akitumia muda wa saa 2:06:26 ambao ulimtosha kumfanya avunje rekodi ya kukimbia muda mfupi zaidi kwenye Olimpiki upande wa Marathoni iliyowahi kuwekwa na Samuel Wanjiru Agosti 24, 2008 ya kukimbia kwa muda wa saa 2:06:32 wakati mashindano ya Olimpiki yalipofanyika Beijing, China.

Katika mbio za leo, Simbu alimaliza katika nafasi ya 17 akitumia muda wa saa 2:10:03 wakati Geay alishindwa kumaliza mbio.

Kilichotokea kwa Geay ni sawa na kilichomkuta gwiji wa Marathoni, Eliudi Kipchoge ambaye alishindwa pia kumaliza kwa kile kinachotajwa ni kutojisikia vizuri.

Kwa ushindi wa jana, Tola anakuwa Muethiopia wa nne kupata medali ya dhahabu katika Olimpiki kwenye mbio za Marathoni akifuata nyayo za Abebe Bikila aliyeshinda mara mbili tofauti na Mamo Wolde.

Katika mbio hizo, Bashir Abdi wa Ubelgiji alishika nafasi ya pili akitumia muda wa saa 2:06:47 na nafasi ya tatu ilichukuliwa na Benson Kipruto wa Kenya aliyetumia muda wa saa 2:07:00.

Kenenisa Bekele ambaye alikuwa miongoni mwa wanariadha waliokuwa wakipewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri kwenye mbio hizo, alimaliza akiwa wa 39 baada ya kutumia muda wa saa 2:12:24.

Kwa kuibuka na ushindi wa medali ya dhahabu katika Marathoni, Tola atapata kitita cha Dola 50,000 (Sh 135 milioni) kutoka shirikisho la kimataifa la riadha (IAAF) ambalo liliahidi kutoa kiasi hicho cha fedha kwa kila mwanariadha atakayeshinda medali ya dhahabu katika Olimpiki mwaka huu.

Chanzo: Mwanaspoti