Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yawatuliza mashabiki

Karabaka Zimbwe Mtale Simba yawatuliza mashabiki

Mon, 12 Aug 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mfungaji wa bao pekee katika mechi ya jana kati ya Simba na Coastal Union, Salehe Karabaka, amewatoa hofu wanachama na mashabiki wa timu hiyo kuwa wasiwe na wasiwasi na timu yao msimu huu kwani itafanya makubwa, akisema ushindi wa bao 1-0 uliopatikana na kushika nafasi ya tatu kwenye Ngao ya Jamii ni mwanzo tu wa shughuli ya msimu mzima.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo huo wa kutafuta nafasi tatu ya michuano ya Ngao ya Jamii jana, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Karabaka alisema ametumwa na wachezaji wenzake kuwaambia wanachama na mashabiki wa timu hiyo hawapaswi kuwa na hofu kwani wapo kwa ajili ya kupambana kuipigania nembo ya Simba.

"Kwa niaba ya wachezaji, ni kwamba tumejiandaa vizuri kwa ligi, Jumapili tunaanza kazi, wajitokeze ndiyo kwanza shughuli inaanza, tunataka kila tunapokwenda kucheza wajitokeze kwa wingi uwanjani ili watushangilie," alisema.

Akizungumzia mchezo huo, alisema ulikuwa mgumu kwa sababu wapinzani wao nao walijiandaa na walionekana wamepania kucheza hiyo mechi kuliko hata ilivyokuwa dhidi ya Azam FC.

Karabaka pia alisema amefurahi kuweka rekodi ya kucheza mechi ya kwanza msimu huu na kufunga bao kama ilivyokuwa kwenye Kombe la Mapinduzi mwaka jana, alipocheza dhidi ya JKU.

"Mwaka jana Kombe la Mapinduzi nilicheza mechi ya kwanza tu baada ya kusajiliwa na Simba, nikafunga bao dhidi ya timu niliyotoka, JKU na leo nimecheza mechi ya kwanza ya msimu nimefunga bao, tena dhidi ya timu ambayo nimeshawahi kuichezea, Coastal Union, hii ni rekodi yangu nzuri sana kama mchezaji," alisema Karabaka ambaye alikuwa mwiba kwa mabeki wa timu pinzani jana.

Alifunga bao hilo dakika ya 10 ya mchezo, baada ya kazi kubwa iliyofanywa na wachezaji kadhaa wa Simba.

Mpira ulianzia kwa beki wa kulia Kelvin Kijili, ambaye alipanda nao kwenye wingi ya kulia, akapiga krosi katikati iliyomkuta Joshua Mutale ambaye naye aliipeleka kwenye wingi ya kushoto alikokuwa Steven Mukwala, kisha akaukokota mpira akiwa pembeni kabla ya kupiga krosi iliyomkuta mfungaji akiwa katikati ya wachezaji wanne wa Coastal Union, akawazidi ujanja na kuuweka wavuni.

Timu zote mbili zililazimika kucheza mechi hiyo ya kusaka mshindi wa tatu baada ya kufungwa mechi zilizopita, Alhamisi, Coastal ikibamizwa mabao 5-2 dhidi ya Azam na Simba ikafungwa bao 1-0 dhidi ya Yanga.

Katika mechi ya jana, Simba ilitawala robo tatu ya mchezo huo, huku Coastal ikionekana kuzinduka dakika 20 za mwisho.

Mukwala alikosa bao la wazi dakika ya 21, alipomegewa pasi na Jean Charles Ahoua, lakini shuti lake lilitoka nje kidogo ya lango.

Nusura Coastal wasawazishe bao dakika ya 32, wakati Jackson Shiga alipomwacha Mohamed Hussein 'Tshabalala' na kupiga krosi iliyotua kichwani mwa Deusdedit Cosmas, ambaye alipiga kichwa akiwa huru, lakini kiliishia mikononi mwa kipa, Moussa Camara.

Coastal ilifanya shambulizi la kushtukiza langoni mwa Simba. dakika ya 41, lakini shuti la Ramadhani Mwenda lilikwenda nje ya lango.

Kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko kadhaa, Simba ikionekana kufanya mengi zaidi kwa kuwatoa Debora Fernandes Mavambo, Ahoua, Mukwala, Tshabalala na kuwaingiza, Valentino Mashaka, Valentine Nouma, Kibu Denis na baadaye aliingia Fabrice Ngoma ambaye alitolewa nje kwa kadi pili ya njano iliyoambatana na nyekundu dakika sita kabla ya pambano kumalizika na mwamuzi Ramadhani Kayoko baada ya kumfanyia madhambi Harnest Malonga.

Cosmas hakuwa na bahati kwani dakika ya 55 alipiga kichwa kingine kilichotokana na mkwaju wa faulo, lakini mpira uligonga nguzo ya pembeni kabla haujaokolewa na mabeki wa Simba.

Kipa Camara alifanya kazi ya ziada dakika ya 68, alipookoa hatari ambayo ingeweza kuipatia Coastal Union bao.

Ngoma alimpasia Nouma bila kuangalia kama mtu anayekuja, kabla hajamfikia, Bakari Selemani akaupitia na kubaki yeye na kipa, lakini shuti lake liliokolewa kwa mguu na kipa Camara, ambaye pia jana alionyesha uwezo mkubwa akiwa langoni.

Baada ya mechi hiyo, timu zote sasa zinajiandaa na ufunguzi wa Ligi Kuu Tanzania Bara itakayoanza Ijumaa, Simba ikitarajia kucheza Jumapili ijayo dhidi ya Tabora United, Uwanja wa KMC, Mwenge, Dar es Salaam, huku Coastal ikisubiri hadi Agosti 29, itakapocheza dhidi ya KMC kwenye uwanja huo huo uliopo Mwenge.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: