Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yawatisha Vipers FC

Simba SC Saikolojia Simba yawatisha Vipers FC

Fri, 24 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kiungo mkongwe, Jonas Mkude, Jimmyson Mwanuke,  Augustine Okrah na chipukizi Mohammed Mussa, wameachwa katika kikosi cha Simba kilichoondoka nchini jana kuelekea Uganda kwa ajili ya kuwakabili wenyeji, Vipers FC kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayochezwa kesho jijini, Kampala.

Msafara wa Simba umeondoka ukiwa na wachezaji 25 na lengo moja la kusaka ushindi ili kurejesha matumaini  ya kusonga mbele katika mashindano hayo ya kimataifa. 

Akizungumza nasi jana kabla ya kusafiri, Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliviera 'Robertinho' alisema tayari amelinasa faili ya Vipers na kujipanga vyema namna watakavyoikabili.

Robertinho alisema anafahamu vyema mchezo huo utakuwa mgumu na wenye ushindani mkubwa kwa sababu kila upande unahitaji pointi tatu ili kufufua 'mwanga' kuendelea na michuano hiyo inayofanyika kila mwaka.

“Ninaifahamu vizuri Vipers, tumewaandaa wachezaji kimbinu, kiufundi na kisaikolojia ili kufikia malengo ya kusaka ushindi katika mchezo huo,” alisema Robertinho.

Kocha huyo aliongeza anatumia ubora na madhaifu ya wapinzani wao kwa ajili ya kutafuta matokeo yanayotarajiwa na mashabiki na wanachama wa Simba yatakayowarejeshea furaha ambayo wanaisubiri.

Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema kikosi cha timu hiyo kipo imara na wameenda Uganda kwa ajili ya kutafuta matokeo chanya tu.

Ahmed alisema mechi hiyo itakuwa ndio fainali yao kutokana na kushikilia mustakabali hatima ya kusonga mbele katika michuano hiyo.

"Tumejipanga, matumaini yetu yote Wanasimba yapo kwenye mechi hii dhidi ya Vipers. Mustakabali wa ushiriki wetu kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa msimu huu utaamuliwa na dakika 90 za pale Entebbe. Sisi kama Simba tumejidhatiti, tutaondoka na alama tatu pale Uganda ili kujiweka sawa kwenye vita yetu ya kuitafuta nusu fainali msimu huu," alisema Ahmed.

Aliongeza kwa kuwapa salamu kutoka kwa Rais wa heshima wa Simba, Mohamed Dewji na Bodi yake ya Wakurugenzi ya kutokata tamaa na kuendelea kushikamana katika wakati huu mgumu na waamini yatakaa sawa.

"Tumeona hata timu mbalimbali barani Ulaya, mfano Liverpool ni mbabe sana, linapokuja suala la mechi za kimataifa za Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini mmeona kilichomkuta dhidi ya Real Madrid. Ni kawaida kwa timu ambayo inayojitafuta na kujitengeneza upya baada ya kutamba kwa muda," Ahmed alisema.

Simba inaburuza mkia katika Kundi D baada ya kufungwa bao 1-0 na Horoya AC ya Guinea na ilikubali kichapo cha magoli 3-0 kutoka kwa Raja Casablanca ilipowavaa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam. 

Chanzo: www.tanzaniaweb.live