Uongozi wa Simba, umeweka wazi kuwa, kukosa penalti kwenye mchezo wa fainali ya Ngao ya Jamii kwa nyota wao wawili, Moses Phiri na Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’ ni sehemu ya mchezo.
Agosti 13, mwaka huu, Simba ilitwaa Ngao ya Jamii kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga. Ushindi wa Simba ilikuwa ni kwa penalti 3-1 baada ya dakika 90 kuwa 0-0.
Kwa wapigaji penalti wa Simba, wawili walikosa ambao ni Phiri aliyeipaisha na Saido ambaye penalti yake iligotea kwenye mikono ya Djigui Diarra.
Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally, ameweka wazi kuwa, hakuna aliyetarajia itakuwa hivyo, lakini imetokea.
“Kwa wachezaji wetu kukosa penalti hiyo sio adhabu kubwa kwao, ni sehemu ya mchezo na huwa inatokea. Kumbuka kwamba hao wote kwenye mchezo dhidi ya Singida Fountain Gate walifunga, ila mbele ya Yanga walikwama.
“Kushindwa kwao ni timu kwa pamoja ndio maana wengine waliofuata walifanya kazi kubwa kutimiza majukumu. Tumefurahi sana kutwaa Ngao ya Jamii, pongezi kwa wachezaji wote bila kumsahau kipa Ally Salim, mikono yake ilikuwa ya dhahabu,” alisema Ally.