Baada ya kupoteza kwenye hatua ya nusu fainali dhidi ya Azam FC katika mchezo wa Kombe la Shirikisho la Azam Sports, hesabu za Simba ni kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya wajeda, Ruvu Shooting.
Timu hiyo chini ya Kocha Mkuu, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ imegotea hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo iliposhuhudia ubao wa Uwanja wa Nangwanda Sijaona ukisoma Azam FC 2-1 Simba.
Kesho Ijumaa, Simba itacheza dhidi ya Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Azam Complex, ikiwa ni mzunguko wa pili ambapo ule wa mzunguko wa kwanza ubao wa Uwanja wa Mkapa ulisoma Ruvu Shooting 0-4 Simba.
Juma Mgunda, Kocha Msaidizi wa Simba, alisema wanatambua ugumu wanaopata kutoka kwa wapinzani wao jambo linalowafanya wachukue tahadhari.
“Kila mchezo unakuwa na mbinu zake na maandalizi kuhusu mechi zetu zote kwenye ligi tunayachukua kwa umuhimu mkubwa kwa kuwa wachezaji wanahaki ya kutimiza wajibu wao,” alisema Mgunda.
Ruvu Shooting ipo nafasi ya 16 ikiwa na pointi 20 baada ya kucheza mechi 27, huku Simba ikiwa nafasi ya pili na pointi 64.