Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yavunja ukimya kocha mpya anayetua Msimbazi

Alexsandre Santos Vsn Kocha Mkuu wa Petro de Luanda, Alexsandre Santos.

Tue, 4 Jun 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Klabu ya Simba imetajwa iko katika mazungumzo na kumwajiri Kocha Mkuu wa Petro de Luanda ya Angola, Alexsandre Santos, ambaye ni raia wa Ureno kwa ajili ya msimu mpya wa mashindano unaotarajiwa kuanza mapema Agosti, mwaka huu.

Tayari Petro de Luanda imethibitisha Santos anaondoka klabuni kwao baada ya kuwaongoza kutwaa ubingwa wa nchi hiyo mara tatu pamoja na Kombe la FA mara moja, ingawa haikuweka wazi wapi ataelekea.

Taarifa kutoka ndani ya Simba zinasema Santos ni mmoja kati ya makocha wanaowaniwa na klabu hiyo kwa muda mrefu, baada ya kumkosa misimu miwili ya nyuma na kuangukia kwa Mserbia Zoran Maki, ambaye hakudumu sana ndani ya kikosi cha Wekundu wa Msimbazi.

Chanzo hicho kilisema Santos pamoja na Florentine Ibenge, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), wanapewa nafasi zaidi ya kuchukua mikoba iliyoachwa na Abdelhak Benchikha.

"Kuna majina ya makocha wengi sana, lakini kwa kiasi kikubwa hawa wawili (Santos na Ibenge), mmoja wao anaweza kupewa mkataba na Simba, kwa sababu ya ukaribu na maelewano na viongozi, mwingine uwezo wake wa ufundishaji unaonekana kuwavutia.

Ibenge, pamoja ni kocha mzuri, ana maelewano mazuri na mabosi, yeye na klabu yake na huyu Mreno mabosi wanavutiwa naye kutokana na uwezo wake mkubwa wa ufundishaji, walimkosa misimu miwili iliyopita kutokana na dau kubwa la kumng'oa, lakini sasa anamaliza mkataba," kilisema chanzo chetu.

Kiliongeza aina ya ufundishaji wa kusakata kandanda ndiyo aina ya soka ambalo Simba wanacheza kama falsafa ya klabu yao inavyojitambulisha.

"Huyu jamaa anafundisha kucheza soka la pasi fupi fupi na kasi na kushambulia mithili ya nyuki, kama ilivyokuwa zamani kwa Milovan Cirkovic au Dragan Popadic, mfano unaona Petro de Luanda kwa misimu ya karibuni ilivyokuwa tishio kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika," alisema mtoa taarifa.

Kocha huyo aliiongoza Petro de Luanda kufika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo ilitolewa na TP Mazembe ya DRC, ilipochapwa ugenini mabao 2-1, baada ya suluhu nyumbani kwao.

Meneja wa Habari wa Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alikiri mchakato wa kumsaka kocha mpya na kusajili wachezaji wapya unafanyika kwa wakati mmoja na kwa umakini.

"Tuna orodha ya makocha wengi sana walioleta maombi yao, wapo watu wanaoshughulika na suala hilo, pia wapo wengine wanaoshughulika na usajili, tukishamaliza mchakato, kila kitu kitawekwa wazi," Ahmed alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live