Kikosi cha Simba kinaendelea kujifua kwa ajili ya mechi ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC) dhidi Ihefu itakayopigwa kesho kwenye Uwanja wa Azam Complex, ambapo benchi la ufundi la Wanamsimbazi hao chini ya Kocha Mkuu Mbrazili, Oliveira Roberto 'Robertinho' wakitumia saa 2 tu kumaliza mipango ya mechi hiyo katika uwanja wa mazoezi wa Mo Simba Arena.
Awali mechi hiyo ilikuwa ipigwe kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini lakini mchezo huo umehamishiwa Azam kutokana na uwanja huo kuwa na matumizi mengine.
Mwanaspoti lilikuwa mubashara katika mazoezi ya jana yaliyofanyika uwanja wa Mo Simba Arena, Bunju kuanzia saa 3:15 hadi saa 5:15 na kushuhudia mbinu mbali mbali na utendaji kazi wa wachezaji 26 waliokuwa mazoezini hapo.
Beno Kakolanya, Ally Salim, Ahmad Feruz, Israel Patrick, Mohamed Hussein, Gadiel Michael, Jimmyson Mwanuke, Henock Inonga, Joash Onyango, Nassoro Kapama, Mohamed Ouattara, Keneddy Juma, Sadio Kanoute, Ismael Sawadogo, Jonas Mkude, Mzamiru Yassin, Peter Banda, Kibu Denis, Pape Sakho, Clatous Chama, Mohamed Mussa, Habib Kyombo, Moses Phiri, Augustine Okrah, Jean Baleke, John Bocco ndio walihudhuria mazoezi hayo huku Aishi Manula na Shomari Kapombe wakikosekana.
Baada ya kufika uwanjani hapo, wachezaji walianza kunyoosha viungo na kupasha misuli joto chini ya kocha wa viungo Kelvin Mandla wakati huo Robertinho na wasaidizi wake, Juma Mgunda na Ouanane Sellami walikuwa wakipanga mipango ya namna ya kuanza mazoezi ya mbinu.
Hata hivyo baada ya dakika 15 zoezi hilo lilitamatika na kuhamia katikati ya uwanja na kugawa timu tatu ambazo zilicheza kila kundi kwa kupigiana pasi, kutafuta nafasi na kukaba zoezi ambazo lilitumia kama dakika 15 tena na baada ya hapo kupumzika kidogo kwa kunywa maji kwa wale ambao hawajafunga.
Wakati mazoezi hayo yote yakifanyika, Okrah yeye alikuwa na programu yake maalumu ya kukimbia kwa kuzunguka uwanja katika huku Moses Phiri akiwa amekaa nje akiendelea kupewa matibabu ya mguu wake wa kulia ambao hata hivyo amesema hajaumia sana bali alihitaji utulivu ndio maana akakaa nje na kuweka barafu kwenye mguu huo.
Baada ya mazaezi hayo ya kupiga pasi, kutafuta nafasi na kukaba, Robertinho aliwaita kati wachezaji wake n kugawa timu mbili kisha kuanza kucheza kama mechi na wakati huo, Mkude, Feruz, Ouattara, na Kanoute waliungana kukaa nje na kina Phiri na Okrah aliyemaliza programu yake na wengine kuendelea kukichafua.
Mazoezi hayo ambayo yalikuwa na ushindani mkubwa baina ya timu mbili alizogawa Robertinho, yalikuwa na ushindani wa aina yake kutoka kwa wachezaji na muda mwingi Robertinho, Mgunda na Sellami walionekana kuwaelekeza wachezaji na kubadili mbinu mara kwa mara.
Katika mazoezi hayo yaliyodumu kwa zaidi ya dakika 90 kutokana na mazoezi ya hapa na pale, Chama, Kibu, Saido, Inonga na Sakho ndio walionekana kucheza kwa ubora wa juu katika maeneo yao sambamba na kipa Kakolanya aliyeokoa mashuti mengi ya mastaa hao.
Baada ya mechi hiyo, Mwanaspoti lilizungumza na Robertinho na kuweka wazi mipango yake juu ya mechi na Ihefu huku akisema anahitaji kushinda na timu iko tayari kufanikisha hilo.
"Tunamuda kidogo wa kujiandaa dhidi ya Ihefu lakini tunaamini tutafanya vizuri katika mechi mbili tutakazo kutana nao hivi karibuni. Ihefu ni timu bora lakini kwakuwa hii ni mechi ya mtoano basi tutahitaji kushinda mbele yao ili kusonga mbele," alisema Robertinho na kuongeza.
"Haya ndio mazoezi ya mechi na kama mlivyoona wachezaji wamefanya vizuri na wako katika ari nzuri ya upambanaji hivyo ni matumaini yangu kuwa kufika muda wa mechi tutakuwa vizuri na kucheza kutafuta ushindi."
Aidha kocha huyo amezungumzia kurejea kwa Okrah lakini amesema bado anahitaji muda zaidi ili kuwa fiti na kurejea kwenye makali yake.
"Okrah ni mchezaji mzuri, aliumia na kukaa nje kwa muda mrefu lakini sasa amerudi, hatutaki kumpa presha kwa kumuharakisha bali tumempa muda wa kujifua na akiwa tayari nitamtumia katika mechi zijazo," alisema.
Mshindi wa mechi kati ya Simba na Ihefu atatinga nusu fainali na huko atacheza na Azam iliyotinga hatua hiyo mwanzoni mwa wiki hiii baada ya kuichapa mabao 2-0 Mtibwa Sugar mabao yaliyofunga na Kipre Junior na Abdul Seleman 'Sopu'.