Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yatuma fundi Mwanza

Simba Mwanza Fundi.jpeg Simba yatuma fundi Mwanza

Sat, 24 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Baada ya kubanwa na Kagera Sugar ugenini kwenye Uwanja wa Kaitaba juzi, mabosi wa Simba wameonekana kukerwa na matokeo hayo na fasta wamemkatia tiketi ya ndege fundi mwingine ili kwenda kuongeza nguvu.

Simba itakuwa na mchezo mwingine mgumu ugenini kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza Desemba 26 dhidi ya KMC, iliyo na kumbukumbu ya kutoka nayo sare ya mabao 2-2 katika mechi yao ya mzunguko wa kwanza iliyopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Mabosi wa Simba walifanya kikao kizito na aliyekuwa kocha wao msaidizi Selemani Matola aliyebadilishiwa majukumu kuwa Mkurugenzi wa Ufundi ndani ya timu za vijana na mwishoni mwa mazungumzo walikubaliana fundi huyo aende Mwanza haraka.

Baada ya makubaliano na Matola jana usiku, alitakiwa kukwea pipa kwenda Mwanza kuungana na timu na ataonekana katika benchi kwenye mechi dhidi ya KMC.

Sababu ya Matola kwenda Mwanza kuongeza nguvu kwenye benchi la ufundi inaelezwa mabosi wa Simba hawakupenda kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wa timu yao kwenye sare ya bao 1-1 dhidi ya Kagera, juzi.

Matola anatakiwa kuwepo Mwanza na kupata siku tatu za kushiriki mazoezi ya pamoja na wachezaji huku akishauriana baadhi ya mambo na benchi la ufundi kwani zaidi ya mwezi mmoja alikuwa mbali nao.

Matola alikuwa mbali na benchi la ufundi hata mazoezini hakuonekana kwani alikwenda kusoma Zanzibar kozi ya leseni ‘A’ ya ukocha ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), na mara baada ya kurejea alibadilishiwa majukumu.

Baada ya kuungana na timu, Matola atafanya kazi kwa pamoja na kaimu kocha mkuu, Mgunda na Mussa Hassan ‘Mgosi’ aliyepandishwa kutokea timu ya vijana na alipewa nafasi hiyo wakati Matola yupo masomoni.

“Anatakiwa haraka sana kwenda Mwanza kuungana na timu, kesho asubuhi (leo), anatakiwa kuwa mazoezini, awali mabosi wa Simba waliamini timu inaweza kwenda bila yeye ndiyo maana baada ya kutoka masomoni alikuwa tu Dar es Salaam akisubiri kuanza majukumu yake mapya ya Ukurugenzi Januari, lakini wameona kuna shida na anatakiwa kwenda kuongeza nguvu, unajua Matola ni fundi sana,” kilisema chanzo cha uhakika kutoka Simba.

Mwanaspoti lilipomtafuta Matola alijibu kwa ufupi: “Nipo kwenye kikao kidogo tuongee baadaye.” Wakati huohuo, kuna taarifa kutoka kwenye vyanzo tofauti kwamba uongozi wa Namungo umekuwa ukifanya majaribio ya kupata saini ya Matola ili aende kuboresha benchi lao la ufundi.

Namungo inapambana kumpata Matola kwenda kufanya kazi na wazawa wenzake wawili, Denis Kitambi aliyejiunga kikosi hicho hivi karibuni pamoja na Shedrack Nsajigwa.

Chanzo: Mwanaspoti