Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yatua kwa viungo wawili Yanga

Saiki Simba yatua kwa viungo wawili Yanga

Wed, 26 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Baada ya mazungumzo ya muda mrefu, Simba Queens inadaiwa kufanikiwa kuwashawishi viungo wawili wa Yanga Princess ambao ni wachezaji muhimu kwenye kikosi hicho, Saiki Atinuke na Precious Christopher ili waitumikie msimu ujao wa Ligi Kuu ya wanawake.

Wachezaji hao wamemaliza mikataba na Yanga na timu hiyo haijawaita mezani kuzungumza nao juu ya mikataba mipya, jambo lililowapa upenyo Simba kuingilia kati ili waitumikie.

Inaelezwa viongozi wa Simba wamechungulia mikataba ya awali ya wachezaji hao wa kigeni na kiasi walichokuwa wanalipwa kisha kuwapelekea ofa.

Ikumbukwe Simba inauhitaji kwenye eneo la kiungo mshambuliaji ambalo inaamini kumsajili Precious itakuwa imelamba dume kutokana na uwezo wake wa kuchezesha timu na kupiga pasi sahihi ilhali pia akitumia mguu wa kushoto.

Kwa upande wa Saiki litakuwa chaguo sahihi kwenda kusaidiana na Vivian Corazone ambaye inadaiwa lengo la Simba ni kuleta ushindani kwenye eneo hilo.

Taarifa ilizonazo Mwanaspoti ni kuwa mawakala wanaowasimamia na wachezaji hao hawajaondoka nchini na kinachosubiriwa kwa sasa ni kusaini mikataba.

Akizungumza na Mwanaspoti mmoja wa viongozi wa Simba Queens aliyeomba hifadhi ya jina lake amesema: "Kwa sasa tunamalizana na usajili wa timu kubwa kwa kuwa macho yote yapo huko, lakini hadi wiki ijayo kila kitu kitakuwa sawa."

Kama wachezaji hao watasajiliwa na Simba inaelezwa watalipwa mshahara wa Sh700,000 kwa mwezi kila mmoja na Sh15 milioni za usajili.

Chanzo: Mwanaspoti