Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yatoa sababu ya kukubali kichapo cha Yanga

Tano Ta Yanga Simba yatoa sababu ya kukubali kichapo cha Yanga

Thu, 9 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi akisema ushindi wa mabao 5-1 walioupata dhidi ya Simba juzi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam hauwezi kuamua kitu chochote kuelekea kwenye ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Kocha wa Simba, Robertinho Oliveira, amesema kipigo hicho ni sehemu ya soka na kuongeza kuwa wachezaji wake walipoteza umakini wa kuzuia kipindi cha pili.

Hata hivyo, wakati makocha hao wakisema hayo, Mjumbe wa Baraza la Ushauri la Klabu ya Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu', amesema timu yao imecheza ovyo na matokeo hayo hayaleti picha nzuri kwenye klabu hiyo, huku Ismail Aden Rage akiwasifu Yanga kwa kufanya usajili mzuri wa wachezaji bora na vijana.

Katika mchezo huo mabao ya washindi, mawili yalifungwa na Maxi Nzengeli, Kennedy Musonda, Stephane Aziz Ki na Pacome Zouzoua, huku bao pekee la Simba likifungwa na Kibu Denis akiunganisha kona ya Saido Ntibazonkiza.

"Kipindi cha kwanza Simba walikuwa vizuri, dakika 45 ya kipindi cha pili niliwaeleza wachezaji wangu kucheza mpira, kuhusu ubingwa sasa ni mapema sana kuzungumzia, ushindi huu huuwezi kuamua kitu katika mbio za ubingwa.

"Tunatakiwa kupambana kushinda kila mchezo uliyopo mbele yetu na sasa tunarejea katika uwanja wa mazoezi kujiandaa na mchezo wetu ujao," alisema Gamondi.

Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Simba, Robertinho alisema kipigo cha mabao 5-1 walichokipata kutoka kwa watani wao, Yanga ni sehemu ya mpira.

Alisema kipindi cha pili walipoteza umakini na kushindwa kuzuia nafasi ambazo wapinzani wao ambao walizitumia vizuri.

"Hatukuwa vizuri wakati wanapopoteza mpira na wapinzani walitumia mwanya huo.

"Nawapongeza wapinzani kwa ushindi hatukuwa vizuri hasa kipindi cha pili baada ya kumpoteza Kibu uwanjani, lakini huu ni mpira na tunajipanga kwa mchezo ujao,” alisema Robertinho.

Kaburu, Rage Naye Kaburu alisema anakubali kufungwa na mtani wake Yanga, lakini mabao matano ni mengi sana.

"Niwapongeze Yanga kwa ushindi, goli tano ni nyingi na ni nyingi sana, nadhani viongozi wataongea, mimi kama mwanachama na shabiki nimeangalia mpira tumecheza ovyo tumefungwa, tumekubali matokeo, viongozi watajipanga. Tumecheza ovyo," alisema Kaburu.

Mjumbe mwingine, Rage yeye alisema timu yake imefungwa mabao mengi, na anachokiona ni kwamba Simba haikuwa makini kwenye usajili, huku akiisifu Yanga kwa kufanya usajili bora wa maeneo yenye mapungufu, lakini ikiwa na wachezaji wengi vijana.

"Mara ya mwisho kuifunga mabao 5-0 Yanga mimi ndiyo nilikuwa kiongozi Simba, nadhani tatizo hatukuwa makini kwenye usajili, wenzetu wana timu nzuri na wachezaji wao wengi ni vijana sasa," alisema Rage.

Beki wa Yanga, Dickson Job alisema wamefurahia ushindi huo kwa sababu wamelipa kisasi baada ya kufungwa kwenye mechi ya fainali ya Ngao ya Jamii.

"Tumeshinda mechi ya dabi kwa mabao mengi na tumepata pointi ambazo zimetufanya kuongoza ligi na tumewaonesha kuwa sisi ni bora zaidi yao," alisema Job.

NzengeliMfungaji wa mabao mawili kwenye mechi hiyo, Nzengeli alisema bado wana kazi kubwa ya kufanya katika michezo iliyopo mbele yao na watahakikisha wanashinda na kufikia malengo yao ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

"Mechi ilikuwa ngumu na yenye presha sana, jambo zuri ni kwamba tumeshinda mabao 5-1, lakini sasa tunatakiwa kusahau haya matokeo na kuomba Mungu kusaidia kufanya vizuri katika michezo yetu ijayo, kumfunga Simba ni kuweka heshima tu, kazi kubwa kutafuta ubingwa," alisema Nzengeli.

MANAHODHA SIMBA, YANGA Nahodha wa Yanga, Bakari Mwamnyeto, yeye alishangazwa na timu ya Simba kuruhusu mabao mengi kirahisi katika mechi ya dabi, kitu ambacho hakukitarajia.

"Ni ushindi mkubwa kama ukubwa wa mechi yenyewe, dabi imechezeka, lakini ndiyo kama hivyo mpinzani wetu karuhusu mabao mengi zaidi kwa hiyo dabi imekosa kidogo uzuri na ule utamu wake kwa sababu haikuwa na mzani sana kama siku zote, lakini kwetu sisi tunajipongeza.

“Katika mechi hii wakati wa mapumziko tukiwa bao 1-1, tuliambizana ndani kwamba wapinzani wetu wameshapata bao, basi tulinde kwanza tusiwe na haraka ya kwenda mbele kuwashambulia maana Simba ni timu kubwa ujue kama ilivyo sisi hapa tuliambizana tutulie kwanza kama ni mabao tutayapata baadaye na kweli ikawa hivyo.

Naye Nahodha Msaidizi wa Simba, Mohamed Hussein 'Tshabalala', alisema mpinzani wao alikuwa bora na waliingia wakiwa na mfumo tofauti na ule uliozoeleka, hivyo wakawachanganya.

"Nafikiri tumejitahidi kucheza kwa maelekezo ya mwalimu, lakini nafikiri ‘plani’ haikufanya kazi, ila maelekezo yalikuwa kama tulivyotakiwa kuyafanya, nadhani mpinzani wetu alikuwa bora zaidi na ameweza kutuadhibu.

“Wenzetu walikuwa na plani ya kuwa na viungo wengi katikati ya uwanja na hicho ndicho kilichotuvuruga kwa sababu kila mtu anafahamu aina yao ya uchezaji ni watu wanaotumia zaidi mawinga, lakini leo hawakucheza hivyo, hawakuwa na mawinga asilia, walikuwa na mawinga viungo, hilo ndilo lililotuchanganya, wakawa wengi kati, plani yetu ikafia hapo na tulichelewa kulitambua, baadaye walimu walilitambua hilo tukarekebisha pamoja na hayo tukaambulia matokeo mabaya." alisema Tshabalala.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: