Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yatenga bajeti nono

D240cd1c9cb1f33248f0a787b48ea3d2 Simba yatenga bajeti nono

Mon, 16 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KLABU ya Simba imetenga bajeti nono kukiandaa kikosi chake kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika itaanzia hatua ya awali kwa kucheza dhidi ya Plateau United ya Nigeria katika mchezo wa kwanza utakaopigwa ugenini baadae mwezi huu kabla ya kurudiana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam mwezi ujao.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Mohammed Dewji ‘Mo’ bila kuitaja, alisema bajeti hiyo ni kubwa na haihusiani na michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

“Shabaha yetu ni kufanya vyema kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika safari hii, ili kufika huko tumetenga bajeti inayojitegemea sambamba na motisha watakayopewa wachezaji watakapofanya vizuri katika mechi hizo, “ alisema Dewji.

Dewji alisema baada ya kuwajua mpinzani wao, sasa wanajipanga upya wakijua changamoto gani walizopata msimu uliopita na kutolewa katika raundi ya mwanzo kabisa.

“Tumeshamjua mshindani wetu, tunaenda katika mashindano tukiwa na rekodi mbaya ya kutolewa mapema msimu uliopita na UD Songo ya Msumbiji, sasa tunajipanga vizuri kuwakilisha nchi vizuri,” alisema Dewji.

Alisema wanaenda kuanzia ugenini wakiwa na faida ya wenyeji kucheza mchezo huo wakiwa bila mashabiki wao kutokana na ugonjwa wa covid-19 hali ambayo itapunguza presha kwa wachezaji wa Simba.

“Na tukaporudi kucheza nyumbani taarifa njema ni kwamba mashabiki wataruhusiwa kuingia nusu ya uwanja, hii itakuwa faida kwetu kwani tutakuwa nyumbani hivyo ni fursa kwetu kupigania ushindi,” alisema.

Pia alisema wana mpango wa kuandika barua kwenda Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuomba waruhusiwe kuongeza idadi ya wachezaji wa kigeni watatu kuwatumia kwenye michuano hiyo.

“Kuelekea kwenye dirisha dogo tutafanya usajili wa wachezaji baada ya Gerson Fraga kuumia na tunataka mchezaji wa kumbadili, lakini pia tutaandika barua kwenda TFF kuomba kuongeza wachezaji zaidi ya 10 ili kuwatumia katika michezo ya kimataifa,” alisema.

Aidha, Dewji Alisema Ligi Kuu ina ushindani na kudai pamoja na hujuma zinazoendelea bado wanaendelea kusimama kwenye shabaha yao ya kupambana kuhakikisha wanatetea ubingwa wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Chanzo: habarileo.co.tz