Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yatawala ubingwa bara

Chama Na Matola Selemani Matola na Chama

Mon, 13 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

JANA tuliishia sehemu iliyoonyesha Simba imerejea jijini Dar es Salaam kutoka Misri na kupokewa kwa vaibu la aina yake, japo baadhi ya mashabiki wa klabu hiyo walifariki dunia na na wengine kujeruhiwa wakati wa mapokezi hayo.

Pia tuliona timu ilipofika Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru) na kupokewa na umati wa watu waliojazana kusubiri kuwaona mashujaa wao ambapo kwa haraka sana, Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, ndiye aliyekuwa mgeni rasmi kwenye shughuli hiyo.

Leo tunaendelea na Seleman Matola aliyefanya mahojiano maalumu na Mwanaspoti akifunguka mambo mengine ikiwamo kueleza jinsi walivyopata wakati mgumu wa kuzunguka uwanjani hapo kutokana na idadi kubwa ya mashabiki waliojazana.

Anasema kulikuwa na wakati mgumu, lakini hatimaye walifanikiwa kuingia uwanjani na kupokelewa kwa shangwe na kuelezea kilichofuata baada ya hapo. Endelea naye...!

MWINYI AWAPA TANO

Matola anasema baada ya kufika pale uwanjani, Mwinyi alipewa nafasi ya kuzungumza na kuwapongeza mastaa wa Simba huku mashabiki wakishangilia kwa nguvu kubwa kutokana na jinsi alivyokuwa anaongea kuonyesha kuwa amefurahishwa na matokeo yale.

“Pamoja na marais wote wa nchi hii kupenda michezo, ukweli Mwinyi alikuwa mpenzi mkubwa wa michezo, hata ukiangalia utaona kuwa alielezwa haraka awe mgeni rasmi na hakusita, alikuwa kati ya marais wachache sana wa Afrika ambao walikuwa wapenzi wakubwa wa soka.

“Alizungumza mambo mengi, lakini moja ya jambo ambalo alilisema ni kwamba bado kazi haijamalizika, alirudia zaidi ya mara tatu kusema neno hilo akiwa anamaanisha kuwa tunatakiwa kuongeza juhudi na tusiamini kuwa tunaweza kufika mbali kwa urahisi.

“Alitueleza tunatakiwa tukitoka hapo tufahamu kuwa kazi ndiyo imeanza, tuongeza juhudi kwenye maandalizi, tuanzie pale tulipoishia kwenda mbele na mashabiki walifurahi sana.”

WAJAZWA MINOTI

“Sina kumbukumbu sana lakini ninachokumbuka tulipewa fedha, tulipotoka pale tulienda hotelini viongozi wa Friends walitupa hela sikumbuki vizuri ilikuwa shilingi ngapi kila mmoja lakini ilikuwa hela nzuri kwa wakati ule.

“Viongozi nao walikuwa kama Mwinyi tu alivyosema, walipata hofu kuwa tunaweza kulewa sifa na kuacha majukumu yetu ya msingi ya kujiandaa kwa ajili ya hatua ya makundi ambayo ilikuwa muhimu sana na kutusisitiza tunatakiwa kuweka akili yetu kwenye hatua inayofuata kwa kuwa ngumu zaidi pia, kumbuka hapa ndiyo tumeingia makundi na kila mmoja anatoa macho kweli kweli.

“Nchi nzima kipindi kile ilitupongeza na ni ishu ambayo ilibaki kuwa gumzo kwa muda mrefu, lakini shida kubwa ilikuja kwenye kutoka pale kwenda mbele ndiyo ilikuwa shughuli kwani hatukufanya vizuri sana kama wengi walivyokuwa wanatarajia.

WAANZA TIZI LA MAKUNDI

Matola ambaye hajasafiri na Simba kwenda Guinea kwa kuwa anaendelea na masomo yake ya lugha na kompyuta jijini Dar es Salaam, alisema anakumbuka hawakupata muda wa kupumzika walitakiwa kuendelea na mazoezi moja kwa moja na waliendelea kuwa chini ya Siang’a ambaye anasema alijifunza mambo mengi sana kutoka kwa kocha huyo raia wa Kenya.

“Wakati Simba inamleta Sing’a hakuwa kocha mkubwa sana, wengi walimchukulia kama kocha wa kawaida, lakini nataka kukuambia babu alikuwa anajua sana, alikuwa mzuri wa mbinu na timu yake ilikuwa inacheza soka zuri na ilikuwa na ubora wa juu wa kujilinda.

“Mara nyingi alikuwa anaweza kufahamu tatizo la mchezaji hata kabla wachezaji wenzake hajafahamu, alikuwa mzuri sana wa kuzungumza na mchezaji mmoja mmoja, kama kipindi chake hatukufanya vizuri basi ulikuwa uzembe wetu kwa kuwa alikuwa na ubora wa juu sana na wachezaji wake wengi walikuwa na nguvu na kasi ya hali ya juu.

“Nakumbuka tulifanya mazoezi kwa uhuru sana chini ya kocha huyo kwa kuwa pia alikuwa hawezi kuingiliwa na mtu yoyote na mabosi wa Simba walikuwa wanamuacha anaendesha timu yake anavyopenda ndiyo maana wachezaji wengi wakawa washikaji zake.

WARUDISHWA MISRI, WACHEMKA

“Baada ya ratiba kutoka ya hatua ya makundi nakumbuka tulipangwa tena na timu kutoka Misri walikuwa wale jamaa wanaitwa Ismailia, baada ya kupangwa nao kila mtu alianza kupata hofu lakini sisi tukasema tunaruka nao kibabe.

“Sitaki kuzungumza mambo mengi sana hapa, lakini nakumbuka tulienda kwao walitufunga kama sikosei ni 1-0, tuliporudi hapa nyumbani nakumbuka tuliwabana na kutoka nao suluhu, jamaa walikuwa wazuri sana kwa wakati huo nao, walitubana sana tulipokwenda kwao kwa kuwa walishatuona kuwa tumewaaibisha kaka zao, hivyo naweza kusema kuwa fitina ambazo tulizokwepa kwa Zamalek kwao tuliingia mtegoni.

“Watu wengi hawafahamu, lakini sisi tulikutana utamaduni wa Simba haiwezi kufungwa nyumbani kwake dhidi ya timu ya Misri na baadhi ya kumbukumbu zangu zinaonyesha tulishashinda michezo mingine sana hapa nyumbani mfano mwaka 2019: Simba 1-0 Al Ahly

2018 Simba 2-2 Masry, 2010: Simba 2-1 Hodoud, 2003 Simba 1-0 Zamalek 2003, Simba 0-0 Ismaily 2001, Simba 1-0 Ismailia 1996, Simba 3-1 Mokawloun, 1985 Simba 2-1 Al Ahly, 1974 Simba 1-0 Mehalla hizi ni baadhi tu lakini naamini zipo nyingi zaidi.

“Nakumbuka pia tulikuwa na timu moja kutoka Ivory Coast, wale jamaa aliotoka Stephen Aziz KI wa Yanga, Asec Mimosas na El Mereikh ya Sudan, baadaye hatukufanya vizuri kwenye hili kundi tukaondolewa lakini nafikiri hatukufuata maelekezo tu au tulilewa sifa sana kwa kuwa kama ni maandalizi tulifanya vizuri sana.

“Wakati mwingine nafikiri, timu inatakiwa kupewa heshima ile tuliyopewa baada ya kufika mwisho wa safari siyo katikati, kama vile baada ya pale tuliona kuwa tumeshamaliza kazi na kuanza kubweteka, tulikuwa na timu bora sana, lakini ndiyo hivyo tuliondolewa.

WABEBA NDOO YA BARA

“Kipindi hiki nafikiri kilikuwa cha Simba zaidi, tulikuwa vizuri sana kwenye ligi na tulikuwa na wachezaji wengi mastaa nakumbuka Juma Kaseja ndiye alikuwa shujaa sana kwenye timu, lakini kulikuwa na mastaa wengine kama kina George Masatu mmoja kati ya wachezaji waliokuwa wanajiamini sana.

“Tulitwaa ubingwa mwaka 2003 na 2004 na Yanga waliona kama vile hawawezi tena kupambana nasi nakumbuka kuna mechi walituchapa lakini mwisho sisi tulichukua ubingwa, mwaka 2005 walichukua ubingwa mara mbili, na 2006 ambao timu yetu haikuwa vizuri sana, lakini pamoja hatukuwa vizuri nakumbuka tuliwafunga Yanga kwenye mechi zote mbili za 2005, sisi tukarudi kwenye ligi ndogo tukachukua ubingwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live