Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yatabiriwa fainali Afrika

1128c572ddc240c9d91bc72aebd19635 Simba yatabiriwa fainali Afrika

Sun, 11 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

LICHA ya Simba kumaliza michezo ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi kwa kufungwa bao 0-1 kutoka kwa Al Ahly ya Misri, wadau wa soka wameitabiria makubwa.

Ahly walipata bao dakika ya 31 lililofungwa na Mohammed Elshanawy kwa mpira wa krosi iliyookolewa na kipa Aishi Manula kabla ya kumkuta mfungaji akiwa chini.

Matokeo hayo yamepokewa kwa mtazamo chanya na wadau wa soka na kuitabiria makubwa kwani kabla ya hatua ya makundi kuanza ilikuwa haipewi nafasi kubwa ya kufanya vizuri na mchezo dhidi ya Al Ahly wengi walidhani ingefungwa idadi kubwa ya mabao kulingana na historia ya msimu wa 2019/19 katika hatua kama hiyo, ilifungwa na Ahly mabao 5-0 mjini Cairo, Misri.

Simba imefuzu robo fainali baada ya kujikusanyia pointi 13 na kukaa kileleni, huku mechi ya juzi dhidi ya Ahly iliyomaliza ya pili ikiwa ni ya kukamilisha ratiba tu kwani katika mechi tano za awali za hatua ya makundi ilifanya vizuri.

Pia wamemaliza hatua hiyo wakiwa wameruhusu kufungwa mabao mawili pekee na wao kufunga mabao tisa, ikiwa ni rekodi nzuri ya kuonesha Simba ina jambo lake katika hatua za mbele za michuano hiyo.

Kocha wa Zanzibar Heroes, Hababuu Ali alisema ana imani kuwa Simba itacheza fainali kutokana na jinsi wanavyocheza kwani inaonekana ni mkakati wao waliojiwekea kulingana na mpinzani wanayekutana naye.

“Simba ya msimu huu ni nzuri. Unaona timu inavyocheza hata awe ni mchezaji gani yeyote anayepata nafasi ya kucheza anamudu nafasi yake kisawasawa hivyo inacheza kimkakati kila idara ,” alisema.

Naye Mwenyekiti zamani wa Simba, Ismael Aden Rage alisema: “Nafikiri Simba hii itafika mbali, wanaweza kufika fainali kwa mfano wa mechi ya juzi na Al Ahly, Simba ilicheza kwa ufundi, ilitaka heshima na kuonesha yeye ni kinara wa kundi na kaipata.

“Kwenye robo fainali kwa sababu watacheza na washindi wa pili wa makundi mengine haimaanishi watapita kirahisi, lakini kwa namna Simba ilivyo ni timu ambayo msimu huu inakwenda kuendeleza na kuandika historia mpya zaidi kwa soka la Tanzania hapa Afrika.”

Kwa upande wake, kocha mkuu wa Simba, Didier Gomes alisema ubora ambao umeoneshwa na wachezaji kwenye mechi za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, unampa jeuri ya kutohofia timu yoyote Robo Fainali.

Gomes alisema Kundi A, ndilo lililokuwa gumu kuliko yote, lakini vijana wake walionesha ujasiri wa hali ya juu, baada ya kupambana na kumaliza vinara, hivyo haoni kama kuna timu nyingine itakayowasumbua.

“Kama tumeweza kuongoza kundi mbele ya bingwa mtetezi Al Ahly na wazoefu AS Vita sidhani kama kuna timu nyingine inaweza kutusumbua, naheshimu wapinzani wote walioingia

hatua hii, lakini hakuna ubishi Simba ni timu bora Afrika na ipo tayari kucheza na timu yoyote bila hofu,” alisema Gomes.

Simba imefanikiwa kumaliza kinara Kundi A kwa pointi 13 ikifuatiwa na Ahly yenye pointi 11 na timu hizo kusonga hatua ya robo fainali na kuziacha As Vita ya DR Congo na Al Merreikh ya Sudan zikitupwa nje.

Baada ya kukamilika kwa mechi nyingine za makundi ya michuano hiyo, Simba sasa inasubiri kupangiwa mpinzani wake wa hatua inayofuata kutoka katika timu tatu za makundi zilizomaliza nafasi ya pili Aprili 30.

Kundi B iliyomaliza nafasi ya pili ni CR Belouizdad ya Algeria. Kundi C na D lilikuwa likisubiri kumalizika kwa mechi za jana usiku ili kumtambua atakayemaliza nafasi ya pili.

Timu zilizokuwa zikipigania nafasi hiyo katika Kundi C ni Horoya AC ya Guinea au Kaizer Chiefs (Afrika Kusini) wakati za Kundi D ilikuwa ikisubiriwa kati ya MC Alger (Algeria) au Zamalek SC (Misri).

Chanzo: www.habarileo.co.tz