Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yashusha nyota wa Cranes

45e2ef94fd1757065293f30e9ac5d7e7 Simba yashusha nyota wa Cranes

Fri, 4 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

SIMBA imemsajili kiungo wa kimataifa wa Uganda, Taddeo Lwanga kuiongezea nguvu katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kiungo huyo mkabaji wa Uganda The Cranes anakuja kuziba nafasi ya raia wa Brazil, Gerson Fraga ambaye aliumia na atakuwa nje kwa msimu mzima. Mkataba wake umesitishwa kutokana na kuumia huko.

Lwanga aliyewahi kung’ara na timu za Express FC, SCV Kampala, Vipers FC na Tanta FC zote za Uganda, alitambulishwa mbele ya waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Simba, Mwina Kaduguda ndiye aliyemtambulisha kiungo huyo ambaye mkataba wake haukuwekwa wazi ni wa muda gani wala thamani yake.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Klabu ya Simba, Mohamed Dewji ‘Mo,’ inadaiwa ametumia dau la Sh milioni 700 kumbakisha kiungo Clatous Chama.

Chama ambaye mkataba wake ulikuwa ukingoni na alikuwa akihusishwa na Yanga kunyatia saini yake kutokana na ubora wake tangu kujiunga na wekundu hao wa Msimbazi.

Mwenyekiti wa Simba, Kaduguda alisema kutokana na juhudi za kumbakiza Chama, anampongeza Mo. “Natoa pongeze kwa Mohamed Dewji maana kumlipa mchezaji mmoja shilingi milioni 700 ili abaki sio ndugu yako wala mtoto wako. Chama amefanya kazi kubwa waliokuwa wanapiga kelele wamenyamaza,” alisema Kaduguda.

Mbali na hilo, alisema mchakato wa mabadiliko wa klabu hiyo unakwenda kukamilika muda sio mrefu.

Alisema kwenye mabadiliko hapakosi changamoto lakini huwapa ari ya kupambana kufikia malengo waliyojiwekea na walipofikia hawawezi kurudi nyuma.

“Mabadiliko sio jambo la kitoto kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati, Simba tumejitahidi hivyo, lazima tukamilishe,” alisema.

Akizungumzia mchezo ujao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Plateau United, alisema ni moja ya timu nzuri nchini Nigeria hivyo haipaswi kubezwa ila malengo yao ni kupambana kufanya vizuri ili kuvuka hatua inayofuata na kuwahimiza wadau, wapenzi, wanachama na mashabiki kuiombea timu.

Msemaji wa Simba, Haji Manara alihimiza mashabiki wa klabu hiyo kujitokeza kwa wingi uwanjani kwani mashabiki wanaohitajika ni 30,000 hivyo wahakikishe wanajaza wao na sio wa klabu nyingine.

Alisema ikitokea wa klabu nyingine wanakwenda basi wawe wastaarabu wasiwadhuru na kusisitiza kwenda na barakoa kama ambavyo inahitajika kulingana na maelekezo ya Shirikisho la Soka la Afrika (CAF).

Alitaja viingilio vya mchezo huo utakaochezwa saa 11:00 jioni kuwa ni Sh 150,000 Platnum, Sh 40,000 kwa VIP A, Sh 20,000 kwa VIP B na C na mzunguko Sh 7,000.

Manara alisema wageni wao Plateau wanatarajia kuja nchini kesho tayari kwa mchezo huo utakaochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Chanzo: habarileo.co.tz