Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yashusha kifaa kingine

Simba Mussaaaa Simba yashusha kifaa kingine

Mon, 16 Jan 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kikosi cha Simba bado kipo Dubai huku mabosi wa klabu hiyo wameendelea kuimarisha kikosi chao kimya kimya kwa kunasa straika mwingine wa mabao anayeungana na kina Saido Ntibazonkiza na Jean Baleke.

Straika huyo mpya ambaye anasubiri kutambulishwa ni Mohamed Mussa, mmoja wa nyota waliong'ara kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi 2023 iliyomalizika juzi usiku kwa Mlandege kubeba ndoo kwa kuifunga Singida Big Stars kwa mabao 2-1.

Taarifa kutokea ndani ya Simba, zinasema uongozi wa timu hiyo umekamilisha usajili wa nyota huyo aliyefunga bao katika mechi ya ufunguzi wa michuano ya Mapinduzi wakati Malindi ilipoinyoa Jamhuri kwa mabao 2-0 na tayarui mchezaji huyo ameshawaaga wachezaji wenzake ili kuja jijini Dar.

Inaelezwa wakati wa michuano hiyo, mmoja wa Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Simba (jina tunalo), alikwenda hadi nyumbani kwa familia ya Mussa ili kuzungumza na wazazi wake hasa baada ya kuvutiwa na soka lake tamu na kuona anaweza kuifaa timu hiyo katika eneo hilo la mbele.

Mazungumzo ya pande hizo mbili yalienda vyema na ilikubaliwa imchukue Mussa ili ajiunge na Simba na mjumbe huyo aliwafahamisha wenzake dili lilivyoenda na fasta wakampa mkataba wa miaka mitatu ili akitumikie kikosi hicho kitakaporejea kutoka Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Taarifa zaidi zinasema kuwa tayari Mussa amewaaga wachezaji, benchi la ufundi pamoja na makocha kuwa anaondoka katika kikosi hicho baada ya dili lake la kuichezea Simba kwenda vizuri na ameshaondoka siku tatu zilizopita kuja Dar es Salaam ili kuwasubiri wenzake watoke kambi ya Dubai.

"Aliwahishwa Dar kwa ajili ya kutafutiwa viza ya kwenda Dubai ili aungane na wenzake kambini na tayari ameshapigwa picha kabisa akiwa na uzi wa Simba, kilichobaki ni kutambulishwa," kilisema chanzo hicho.

Mbali na kung'ara kwenye michuano ya Mapinduzi, nyota huyo wa Malindi ni kati ya wafungaji wanaoongoza kwa mabao kwenye Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), akiwa na mabao saba hadi sasa.

Kama Mussa akitambulishwa kuwa mchezaji mpya wa Simba inakuwa timu yake ya tatu kuitumikia kwenye Ligi Kuu Bara kwani amewahi kucheza Gwambina chini ya kocha Melis Medo na Mbeya City.

Katibu wa Malindi, Mohammed Masoud alikiri ni kweli Mussa alikuwa na mazungumzo na Simba na kama wamefikia wapi ama kama ameshajiliwa, hilo lipo kwa upande wa Simba na sio klabu yao, kwani wao walishamalizana naye.

"Binafsi naamini Simba yenyewe wataeleza kila kitu kuhusiana na dili hilo la Mussa, kwani jambo hili hali iliyopo sasa wao ndio wenye mamlaka ya kulizungumzia hili kwetu limetoka," alisema Masoud na kuongeza;

"Mussa ni mchezaji mzuri amefanya hivyo akiwa hapa Malindi na naamini kama atapata changamoto nyingine hata hapo Simba kuna kitu atakwenda kukionyesha bila shida yoyote."

Chanzo: www.tanzaniaweb.live