Wakati Klabu ya Simba ikianza kutoa mkono wa heri kwa wachezaji ambao haitakuwa nao msimu ujao, uongozi wa klabu hiyo unatarajiwa kumtoa kwa mkopo straika wake, Pa Omari Jobe, raia wa Gabon aliyesajiliwa katikati ya dirisha dogo la usajili msimu uliomalizika, baada ya kiwango chake kutowaridhisha wanachama na mashabiki wa klabu hiyo.
Taarifa kutoka ndani ya klabu ya Simba zinaeleza kwa sasa juhudi zinafanyika kumtoa kwa mkopo mchezaji huyo kwenda timu yoyote ile, ndani au nje ya nchi, ili nafasi yake ichukuliwe na mchezaji ambaye atakuwa na tija ndani ya kikosi.
Habari zinadai, Simba imeshindwa kuvunja mkataba na mchezaji huyo iliyomsajili kwa mwaka mmoja na nusu kwani itapaswa kumlipa kiasi cha Sh. milioni 200 za Kitanzania, kitu ambacho kimewawia vigumu mabosi wa klabu hiyo.
"Jamaa aliingia mkataba wa mwaka mmoja na nusu, ufanisi wake haujawaridhisha, viongozi walitaka kuvunja mkataba, lakini pesa ni nyingi anazotakiwa kulipwa, na haiwezekani kubaki, sidhani kama kuna mwanachama au shabiki wa Simba anaweza kuwaelewa viongozi Jobe akibaki.
"Kwa hiyo anatafutiwa timu aende kwa mkopo ili ipatikane nafasi ya kusajili straika mwingine, na kwa bahati nzuri klabu mbalimbali ndani na nje ya nchi zinamhitaji, hivyo itakuwa rahisi tu," kilisema chanzo hicho.
Wakati hayo yakiendelea, klabu hiyo imetangaza kuachana na straika, Shaaban Chilunda, ambaye alikuwa anacheza kwa mkopo katika Klabu ya KMC.
Katika kampeni yake ya kutangaza wachezaji inayowaacha kila siku mchana, Simba imeachana na Chilunda aliyesajiliwa mwanzoni mwa msimu akiwa hana timu, ingawa awali alikuwa akikipiga katika Klabu ya Azam FC.
Baada ya kutoonyesha kiwango cha kuridhisha, klabu hiyo ilimpeleka KMC kwa mkopo ambako amecheza mpaka mwisho wa msimu uliomalizika.
Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, amesema bado kuna wachezaji wengi sana wataachwa ikiwa ni kampeni ya kutengeneza Simba mpya.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Ahmed alisema wanafanya mabadiliko makubwa kwa sababu wanataka kujenga Simba bora itakayotikisa msimu ujao.
"Bado sana, tunataka kutengeneza Simba bora zaidi, kwa hiyo tunaachana na wachezaji bora tuliokuwa nao, tunasajili bora zaidi ili twende tukafanye vizuri kwenye malengo ambayo tumejiwekea, hiyo ni asilimia mbili tu, safari hii panga ni kubwa mno, kuna wengine wanafuata mbele na kila utakayoona, mbadala wake atakuwa ni mchezaji wa kiwango cha juu.
"Fikiria kama unaweza kumuacha mchezaji kama Saido Ntibazonkiza ambaye hakuwa mchezaji wa benchi, alikuwa ndiye mfungaji bora wa klabu misimu miwili mfululizo, tafsiri yake ni kwamba maboresho yanayofanyika ni makubwa mno ndiyo maana klabu inapata uthubutu wa kuachana naye, safari hii hatutaki mchezo," alisema Meneja habari huyo.