Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yasalimu amri Manungu, yashindwa kutoa burudani iliyowaahidi Mashabiki

Simba Sare Mchezo umemalizika kwa sare tasa

Sat, 22 Jan 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Dakika 90 zimekamilika katika Dimba la Manungu Complex, pale Turiani Mkoani Morogoro, huku bundi mweusi akiwa ameendelea kusimama mlangoni mwa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba SC.

Baada ya kupokea kichapo cha goli 1-0, kutoka kwa Mbeya City, katika mchezo wake wa Januari 17 Jijini Mbeya, hii leo Simba wamelazimishwa sare ya bila kufungana dhidi ya wakata miwa, Mtibwa Sugar.

Katika mchezo wa leo Simba hawakuwa na madhara katika dakika 45 za kipindi cha kwanza pengine labda kutokana na Ubovu wa Uwanja ambao ulikuwa na maji kutokana na mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia leo.

Pengine Simba waliuhitaji kwa hali na mali ushindi katika mchezo wa leo na ndio sababu ya kuanza na washambuliaji wake wawili, Meddie Kagere na Chris Mugalu.

Kipindi cha Pili, Simba walifanya mabadiliko kwa kuwaingiza Bernard Morisson na Kiungo Clatous Chama ambao waliongeza presha katika lango la Mtibwa lakini ubora wa golikipa Shaaban Kado ndio uliokuwa kikwazo cha Simba kupata goli.

Uwepo wa walinzi waliopata kupita katika klabu ya Simba, Abdi Banda na Ibrahim Ame, ilikua ni kiwazo kingine hasa kwa ubora waliouonesha kukabiliana na washambuliaji wenye uchu wa Simba kama Pape Sakho, Hassan Dilunga, Meddie Kagere, Mugalu na Morisson.

Kwa sare hiyo Simba wanaendelea kukamata nafasi ya pili wakiwa na alama zao 25 baada ya kucheza michezo 12, huku Mtibwa Sugar wakiwa nafasi ya 13 na alama zao 12 wakiwa wamecheza michezo 13.

Simba inazidiwa alama 7 na kinara wa Ligi Kuu kwa sasa ambao ni Klabu ya Yanga

Chanzo: www.tanzaniaweb.live