Katika kuhakikisha kuwa Simba SC inafanya vyema msimu ujao na kubeba mataji makubwa kama Ligi Kuu Bara na kufanya vyema katika michuano ya kimataifa kwa maaana ya Ligi ya Mabingwa Afrika, uongozi wa timu hiyo umeanza kushusha mashine za maana kwa ajili ya msimu ujao.
Tayari Simba SC imeanza kuhusisishwa na usajili wa wachezaji akiwemo kipa wa Al Hilal, Issa Fofana, mshambuliaji wa Al Hilal, Makabi Lilepo na kiungo wa Singida Big Stars, Mbrazil, Bruno Gomes.
Chanzo cha ndani ya Simba SC kimesema kuwa klabu hiyo tayari imeshakamilisha baadhi ya usajili ambao hawataki kuuweka wazi japo tayari imefahamika juu ya Simba kufikia katika hatua nzuri za usajili wa Bruno.
“Simba SC tayari imeshakamilisha baadhi ya sajili zake kwa ajili ya kuhakikisha kuwa msimu ujao wanafanya vyema tena katika michuano ya kimataifa na kuna wachezaji wengi wazuri ambao wataingia Simba SC na watu hawataamini juu ya kile ambacho watakiona.
“Bruno Gomes ni kweli Simba SC wapo katika hatua nzuri za kumalizana na kiungo huyu ambaye ameonyesha uwezo mkubwa sana ndani ya ligi kuu msimu huu.
“Wapo wengine kama Makabi Lilepo lakini pia kumrudisha Luis Miquissone, ambaye ndiye chaguo lao namba moja msimu huu japo hawataki kila kitu kifahamike,” kimesema chanzo hicho.
Kwa upande wa Meneja wa Habari wa Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally kuhusu usajili wa timu hiyo amesema: “Simba msimu huu tutashusha mashine za maana ambazo watu hawajawahi kuziona, utakuwa usajili bora kuwahi kufanyika na hiyo yote ni kwa ajili ya kuhakikisha kuwa msimu ujao tunarudi katika ubora wetu.”