Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yasafiri na Bakhresa Misri

Matola Kusoma Simba yasafiri na Bakhresa Misri

Thu, 9 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Bado tunaendelea na mfululizo wa makala za maisha ya kocha wa soka Selemani Matola ambaye ameweka historia ya kuwa kocha ambaye ametwaa makombe kadhaa makubwa akiwa mchezaji na kuyatwaa pia akiwa kocha kwenye kikosi cha Simba.

Mwanzoni tuliona jinsi ambavyo Matola alitoka kwao Kigoma na kujiunga na Toto kisha Kagera Star, baadaye alifuatwa na Yanga na Simba, akajikuta akitua kwenye kikosi cha Simba baada ya misukosuko mingi sana, ameeleza kuhusu mechi yake ya kwanza akiwa na Simba walipovaana na Yanga na George Masatu akakosa penalti, lakini kwa kuonyesha ujasiri wa hali ya juu Masatu aliomba tena kupiga penalti ya kwanza kwenye zile tano za mwisho na hatimaye Simba wanawatupa nje Yanga, wanafanya sherehe kubwa kambini, je baada ya hapo nini kiliendelea? shuka nayo hadi mwisho.

YASAFIRI NA NDUGU WA BAKHRESSA

Matola anaendelea kusema kuwa baada ya kuwatupa nje Yanga, walifuzu kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho ambapo hawakufanya vizuri sana pamoja na kuwa na wachezaji wengi wenye uzoefu mkubwa.

“Hutukufanya vizuri kwenye shirikisho, ingawa kwangu ilikuwa michuano bora, kumbuka kuanzia kote nilipotoka hapa ndiyo nilikuwa naonja ladha ya michuano ya kimataifa, ninakuwa na uhakika wa kupanda ndege angalau kila baada ya wiki mbili.

“Kwenye michuano hii mechi ninayoikumbuka sana ni ile ambayo tulicheza na Ismailia ya Misri kule kwao, walikuwa na timu bora sana, wakiwa na mastaa kama John Otaka, Mohammed Barakat ambao walikuwa na viwango vya juu.

“Kilichokuwa kinatusaidia ni kwamba, wakati huo Simba walikuwa na viongozi wengi ambao walikuwa wanaiunga mkono timu, mfano nakumbuka wakati tunakwenda Misri, tuliongozana na Jamal Bakhresa ambaye ni mdogo wake na mzee Bakhresa ambaye ndiye alikuwa kama mkuu wetu wa msafara. kwanza alikuwa anajua sana fitna na hizo nchi alikuwa anazifahamu haswa, hivyo mambo mengi alikuwa akitusaidia, sijui yuko wapi siku hizi yule mzee.”

Matola anaendelea kusema kuwa walikutana na jambo la ajabu walipotua kwenye Uwanja wa ndege nchini Misri, kwani walikuwa wakisikia mara kwa mara linatajwa jina la Otaka tu.

“Wenzetu walikuwa mahiri sana kwa wachezaji wao, tulipofika Uwanja wa Ndege kila mmoja alikuwa akimzungumzia Otaka tu, tukakutana na dreva taksi, akatuuliza kama ndiyo tunakwenda kucheza na Ismailia, tukamjibu akatuuliza kama tunamfahamu Otaka, alianza kumwaga sifa zake, dah yaani unaweza kuongopa alisema jamaa ni mkali na ndiye gumzo Misri yote, anajua sana kufunga.

“Tulipokuwa tunatoka nje ya uwanja wa ndege tulikuta tambaraa kubwa limeandikwa John Otaka, ilionyesha ni jinsi gani jamaa walikuwa wakimkubali staa wao, wakati huo ulikuwa ukienda Misri, ukifungwa bao chache sana ni tano na penalti ilikuwa lazima wapewe.

WENZAO WACHAPWA 5-0

“Timu za Misri nyingi zilikuwa zikifuzu kwenye michuano ya kimataifa, nakumbuka tulifika pale Alhamisi na tulitakiwa kucheza Jumapili, Ijumaa tulienda kucheki mechi nafikiri wale jamaa walikuwa wanatoka Burkina Faso, walicheza na timu moja ya hapo Cairo wakachapwa 5-0, tulishtuka sana kwa kuwa tuliona jinsi ambavyo walifanyiwa fitina.

“Tukaenda vyumbani tukiwa tumenywea sana, baada ya hapo tulitazama tena mechi ya kesho yake, jamaa nao walichapwa 6-0, ikawa bado sisi sasa ndiyo kiama kinakuja kwetu na jamaa walisema lazima watupige nyingi kwa kuwa wakati huo walikuwa bora zaidi.

Matola anasema siku yao ya mechi ilifika, walienda uwanjani na kukuta uwanja umejaa mashabiki wengi na jamaa walionekana kupania sana kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo.

“Walianza kwa kutushambulia sana, dakika za mwanzoni tu walipewa penalti ya mangumashi, wakapiga wakakosa bado hawakukata tamaa, Mohammed Mwameja alifanya kazi kubwa ya kuokoa hatari langoni, yalipigwa mashuti makali sana, baadaye yule Otaka wao akafunga, kipindi cha pili wakapiga lingine mechi ikaisha 2-0.

MVUA YANYESHA, WAKOSA USHINDI

Matola anasema baada ya kufungwa mabao mawili ugenini kwao ulikuwa kama ushindi kwa kuwa timu nyingine zilikuwa zimefungwa mabao mengi na hata jamaa waliwasifu kuwa timu yao ilikuwa bora sana uwanjani.

“Tukiwa hotelini tulikuwa na furaha kwa kuwa tuliona jamaa tunawamudu sana, basi tukarudi Dar kujiandaa na mchezo wa pili, kipindi kile ilikuwa mvua ikinyesha kama siku hiyo Simba wanacheza kila mtu anaamini kuwa Simba watashinda, basi siku ya mechi kulikuwa na bonge la mvua na mashabiki wa Simba wakawa wana imani kubwa na ushindi.

“Tulifika Taifa, Uwanja wa Uhuru sasa, tukakuta mashabiki wamejaa pamoja na kwamba mvua ilikuwa bado kubwa, jamaa hawakuwa na hofu waliona kama wanatumudu, kama kuna siku niliona wachezaji wa Simba tunajituma ni siku hiyo nilianza namba sita, tulicheza kibabe na hadi mapumziko tulikuwa tunaongoza 2-0, baadaye mwamuzi aliahirisha mchezo kutokana na mvua kuendelea, tukacheza kesho yake tukashinda 1-0 na kutolewa kwenye michuano, tuliumia sana kwa kuwa kwao ingekuwa ile mvua halafu wanaongoza mbili mechi ingechezwa hadi mwisho.

WAFUZU KLABU BINGWA AFRIKA

Matola anasema mwaka 2003, ulikuwa mwaka wa historia kwao baada ya kufuzu kwa michuano ya Klabu Bingwa Afrika, wakiwa wanatawala kwenye soka la Tanzania kwa miaka mitatu.

“Unajua mara nyingi ni kazi sana kuelewa, baada ya Yanga kutamba mwaka 2000, baada ya hapo hadi 2003, sisi ndiyo tulikuwa tunatawala soka la Tanzania wakati huo Kassim Dewji akiwa ndiye katibu lakini mambo mengi ya timu yakiwa yanasimamiwa na Friends of Simba.

“Tulifanya vizuri kwenye Klabu Bingwa, nakumbuka tuliingia hatua ya makundi, tukacheza na timu moja ya Burkinafaso tukaichapa, tukakutana na timu ya Afrika Kusini nao pia tukawachapa tukawa sasa tunakwenda kukutana na timu bora zaidi Afrika wakati huo, Zamalek, hapa ndiyo historia ya Simba ilipo.

“Zamalek walikuwa bora, walishatwaa ubingwa wa Afrika nafikiri mara mbili na walikuwa na wachezaji wengi mahiri kama Hossam Hassan, Mohamed Barakat, Abuutrika wachezaji wao karibu wote walikuwa timu ya taifa ya Misri.

“Maandalizi yetu hayakuwa ya kitoto kipindi hicho, naweza kusema kuwa moja ya kundi ambalo lilifanya kazi kubwa sana kuhakikisha Simba wanafikia mafanikio haya ni Friends ambayo wakati huo ilikuwa na watu wengi ambao hadi leo wapo kwenye timu kama Mulam Ng’ambi, Crescentius Magori, Salim Abdallah ‘Try Again’, Kassim Dewji, Musley na wengine wengi akiwamo Mohammed Dewji ambaye alikuwa mfadhili wakati huo.

“Hawa jamaa walitumia nguvu yao kubwa sana kwa ajili ya timu na wanastahili heshima yao kwa kweli kwenye mafanikio yale ambayo tuliyapata.

Je nini kitaendelea. Usikose toleo la kesho.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live