Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yarudi njia kuu, Ahoua mdogomdogo

Simbasctanzania 1724924854592.jpeg Simba yarudi njia kuu, Ahoua mdogomdogo

Thu, 29 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Simba ipo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kushinda mechi mbili za awali kwa kishindo na kuvuna pointi sita na mabao saba, na kufanya mashabiki wa timu hiyo kutamba “Chama ndo limerudi njia kuu?”

Simba ilianza kwa kuishindilia Tabora United kwa mabao 3-0 kisha kuizima Fountain Gate kwa mabao 4-0 na kukaa kileleni wakati ligi hiyo ikienda mapumziko ya wiki mbili mara baada ya leo kupigwa michezo miwili inayozikutanisha Kagera Sugar na Yanga na ile ya KMC dhidi ya Coastal Union.

Simba ilitaabika misimu mitatu iliyopita wakati watani zao Yanga wakitwaa taji la ligi na Kombe la Shirikisho. Hata hivyo kasi iliyoanza nayo imewapa matumaini wana Simba ambao angalau huko mtaani hata mtandaoni wana kitu cha kusema japo ni mapema mno.

Unaweza kusema Simba ilipotea njia katika misimu hiyo kuanzia usajili, uongozi na namna ya uendeshaji, na msimu huu imeshtuka na kuamua kurejea kwenye njia iliyoipa mafanikio kwa kuwatumia wazawa, kwani kwa sasa Valentino Mashaka ndiye kinara wa mabao akifunga mawili.

Baada ya msoto wa muda mrefu, mwaka 2017 Simba ilijitafuta kwa namna nyingine na ilijipata.

Iliamua kuwekeza kwa wachezaji wengi wazawa na kuwapa imani ya kupambania na hapo ikawa imepata njia yake ya ushindi. Msimu wa 2017-2018 na 2018-2019 kuendelea Simba iliwaamini wachezaji wengi wazawa na walitoa matokeo chanya. Hapo walisajiliwa kina Aishi Manula, Erasto Nyoni, Shomari Kapombe, Kennedy Juma, John Bocco, Hassan Dilunga na wengineo.

Mastaa hao walijazwa ‘sumu’ kuwa wao ndio muhimili wa Simba na walipambana na kuonyesha ubora. Hapo ndipo Simba mpya ikaanza. Timu ikaanza kupendwa mtaani, ikatwaa ubingwa wa ligi. Kimataifa ikawa habari kubwa na kudumu katika ubora kwa misimu minne mfululizo ikitwaa taji la ligi mara nne na kuweka rekodi kadhaa Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho.

Licha ya kuwa na mastaa wengine bora wa kigeni, lakin Simba ile ilijengwa zaidi na wazawa.

Ilikuwa ukiona kikosihicho hutawakosa wazawa wanne hadi watano walioanza. Kipa utamuona Manula, beki za pembeni Kapombe na Mohamed Hussein, kiungo Mzamiru, Jonas Mkude au Saidi Ndemla, Hassan Dilunga huku ushambuliaji ni Bocco. Licha ya kuwepo kwa kina Clatous Chama, Pascal Wawa na Meddie Kagere lakini wazawa waliongoza kupata nafasi katika kikosi.

Ikumbukwe wazawa hao walikuwa wamemezeshwa ‘sumu’ ya Simba. Kuna namna walikuwa na mapenzi ya dhati na timu hiyo na kujitoa kwa hali na Mali kuhakikisha timu hiyo inafanya vyema na kweli ‘boli lilitembea.’

Huo ndio ulikuwa mhimili mkubwa wa Simba ya kimataifa, Simba ya kampa kampa tena. Simba ya ‘pira biriani’ na Simba tishio Afrika.

Muda umeenda, Nguvu ya wazawa wengi wa Simba ilipungua na wengine kuondoka. Simba ikasajili wazawa kadhaa lakini wakashindwa kumeza ‘Sumu’ ya Simba, wakaonekana wa kawaida na hapo ndipo Simba ikapoteana na kutoa mwanya kwa Yanga kutamba katika misimu mitatu iliyopita.

Msimu huu ni kama Simba imeshtuka na kuamua kurejea kwenye njia yake ya kuanza na wachezaji wazawa.

Ilianza kwa kutafuta kocha anayejua kutengeneza timu na kumpa nafasi mchezaji anayeonyesha ubora na sio majina. Ikampata Fadlu Davies akaja na wasaidizi wake na kweli wanafanya hivyo.

“Huyu kocha yeye haangalii jina, anaangalia ubora wa mchezaji na anachokifanya mazoezini ndipo anatoa nafasi. Ana misimamo mikali na hababaishwi,” alisema moja ya viungo wa Simba akimuongelea kocha Fadlu.

Baada ya Simba kumpata Fadlu ikasajili wachezaji wengi vijana na wazawa wa kutosha. Iliwasajili, Kelvin Kijiri, Abdulrazak Hamza, Yusuph Kagoma, Omary Omary, Awesu Awesu na Valentino Mashaka wakiwa wazawa kati ya wachezaji 13 wapya kikosini hapo.

Wakali hao wamewakuta kina Manula, Ally Salim, Hussein Abel, Zimbwe JR, Kapombe, Mzamiru, Edwin Balua, Kibu Denis, Ladack Chasambi, Salehe Karabaka na hapo wakapata sehemu ya kuanzia.

Kocha Fadlu ni kama amewawashia taa ya kijani wazawa. Anawapa nafasi na wamekuwa wakimlipa.

Mfano, mabeki wa pembeni licha ya kuwepo mgeni Valentino Nouma lakini Zimbe JR, Kapombe na Kijiri wanapata nafasi.

Eneo la beki wa kati, pamoja na kuwepo mgeni Karaboue Chamoe, Hamza amekuwa akitesa hivyo hivyo kwa viungo kina Awesu, Kagoma, Balua wanacheza na kule mbele yupo Valentino anayeongoza kwa mabao.

Haina maana kuwa wageni kina Charles Ahoua, Steven Mukwala, Joshua Mutale, Debora Fernandez na wengine hawana msaada, lakini wazawa wenye ubora ndio imekuwa njia ya ushindi kwa Simba kwa zaidi ya miaka mitano.

Hivyo ndivyo timu nyingi duniani zinajiendesha. Wazawa huwa msitari wa mbele kwenye kuipambania timu.

WASIKIE WADAU

Straika wa zamani wa Coastal Union na Taifa Stars aliyewahi kuifundisha Simba, Juma Mgunda alisema ukiwa na wachezaji wazawa wengi wenye ubora unajiamini katika uamuzi.

“Wachezaji wazawa ni muhimu sana kikosini. Wale tunaongea lugha moja na tunaelewana, hivyo unaweza kujiamini kwani mkiwa vizuri wataweza kupambana na kujitoa zaidi kwa ajili ya timu kwa maana inakuwa ni kama timu yao,” alisema Mgunda.

Staa wa zamani wa Simba, Ramadhan Chombo ‘Redondo’ alisema mara zote wazawa ndio wanazibeba timu.

Mchambuzi wa soka katika gazeti hili, Oscar Oscar alisema mhimili wa Simba na Yanga unahitaji wachezaji wazawa ili kufanikiwa. “Hawa wazawa wanazijua zaidi timu hizi kuliko wageni.,” alisema Oscar.

Chanzo: Mwanaspoti