Dakika 90 za mchezo wa kirafiki wa kimataifa zimemalizika kwenye Uwanja wa Uhuru kwa wenyeji Simba kufungwa bao 1-0 na AS Arta Sola 7 kutoka Djibouti.
Bao hilo la kwanza na la ushindi kwa Arta Solar lilifungwa dakika ya 88, kupitia kwa Manucho baada ya kupiga shuti kali lililomshinda kipa wa Simba, Ally Salim.
Kipindi cha pili kilianza kwa Kocha wa Simba, Zoran Maki kufanya mabadiliko ya kumtoa kiungo wake mshambuliaji, Moses Phiri na nafasi yake kuchukuliwa na Dejan Georgijevic.
Mabadiliko hayo yalilenga zaidi kuongeza ufanisi kwenye eneo la ushambuliaji ambalo kipindi cha kwanza lilionekana kutokuwa na madhara licha ya kutengeneza mashambulizi mengi.
Simba iliendelea kulishambulia lango la AS Arta ambapo licha ya kutengeneza mashambulizi mengi yenye hatari ila ilishindwa kuyatumia vyema.
Simba iliendelea kufanya mabadiliko baada ya kuwatoa Israel Mwenda na nafasi yake kuchukuliwa na Abubakar Khamis huku Sadio Kanoute akimpisha Omary Mfaume.
Zoran aliendelea kutoa nafasi nyingine kwa vijana baada ya kumtoa Peter Banda na kumuingiza Hamim Mussa huku pia akitoka Augustine Okrah na kuingia Hassan Kasim.
Victor Akpan alitolewa pia na nafasi yake kuchukuliwa na Pascal Yasata huku Nelson Okwa akitoka na nafasi yake kuzibwa na Hassan Mussa.
Mabadiliko hayo yaliifanya Simba kuendelea kutawala mchezo huku wapinzani wao wakitengeneza mashambulizi machache ila yenye hatari.
Kipigo hicho kwa Simba ni cha pili mfululizo baada ya Agosti 31 kufungwa bao 1-0 na Al Hilal ya Sudan.
Baada ya mchezo huu Simba itarejea kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya KMC itakayopigwa Jumatano hii ya Septemba 7, saa 1:00 usiku katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Kikosi cha Simba kilichoanza ni Ally Salim , Jimmyson Mwanuke, Israel Patrick, Erasto Nyoni, Nassor Kapama, Victor Akpan, Peter Banda, Nelson Okwa, Moses Phiri, Sadio Kanoute na Augustine Okrah.
Wachezaji wa akiba ni Ahmed Feruzi, Hassan Kasim, Abubakar Khamis, Pascal Yasata, Omary Mfaume, Hassan Mussa, Hamim Mussa na Dejan Georgijevic.