Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yapewa marefa wa 8-0

Marefa Pic Data Simba yapewa marefa wa 8-0

Sat, 22 May 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

SIMBA wana matumaini ya kusonga mbele kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kutokana na historia na bahati yao dhidi ya marefa wawili waliopangiwa na CAF. Marefa hao waliwahi kuwachezesha mechi mbili tofauti Jijini Dar es Salaam na jumla yake wakapata mabao 8-0. Refa wa kati aliyepangwa kuchezesha mechi hiyo ya Jumamosi, Pacifique Ndabihawenimana msimu wa 2018/2019 alichezesha mechi baina ya Simba na Mbabane Swallows katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Novemba 28, 2018 ambayo Simba waliibuka na ushindi wa mabao 4-1.

Lakini refa wa mezani, Georges Gatogato ambaye naye anatokea Burundi kama ilivyo kwa Ndabihawenimana, ndiye alichezesha mechi ya marudiano ya raundi ya pili Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu dhidi ya FC Platinum katika Uwanja wa Benjamin Mkapa ambayo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 4-0, licha ya kwamba Wazimbabwe hao waliondoka wakilalamika kwa madai kwamba Mnyama alibebwa lakini hawakuwa na uthibitisho wowote.

Ukiondoa wawili hao, refa msaidizi namba moja aliyeteuliwa na CAF kumsaidia Ndabihawenimana ni Emery Niyongabo na msaidizi namba mbili ni Pascal Ndimunzigo ambao wote wanatoka Burundi.

Simba wanahitajika kupata ushindi wa kuanzia mabao 5-0 au zaidi ili waweze kuitupa nje Kaizer Chiefs na kutinga hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu. Pamoja na mlima huo mrefu unaowakabili Simba, Jumamosi, uongozi wa timu hiyo umetamba kuwa bado una matumaini makubwa ya kuitupa nje Kaizer Chiefs na kusonga mbele.

“Kauli mbiu yetu ni ‘Ama zetu Ama zao, do or die season two’. Tunaamini kama wachezaji wetu watajitoa kwa zaidi ya asilimia miamoja na wakafuata maelekezo ya kocha, nina imani tutawatoa Kaizer Chiefs.

Safari hii hatutaki suala la tumejitahidi. Tunatakiwa kuwatoa Kaizer Chiefs. Uongozi umejipanga vizuri na ni jukumu la wachezaji lililobakia. Waende uwanjani wakavuje jasho,” alisema Manara.

Manara alisema kuwa soka ni mchezo wenye matokeo ya kushangaza hivyo wanayo matumaini ya kupindua meza hapa Dar es Salaam. Katika hatua nyingine Simba imetangaza viingilio vya mechi hiyo huku ikimtangaza mkuu mpya wa mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla kuwa mgeni rasmi wa mechi hiyo.

Uongozi wa Simba umeomba kwa CAF waongezewe idadi ya mashabiki kutoka 10,000 wa mwanzo hadi 20,000 au 30,000 hivyo ndio wanasubiria majibu. “Tunaamini watatukubalia kwa hilo ukizingatia kwa sasa hali ya Corona imepoa kidogo ba baadhi ya nchi mashabiki wameanza kuingia viwanjani,”aliongeza Manara.

Viingilio katika mchezo huo vitakuwa ni Sh 40,000 kwa VIP A, Sh 25,000 kwa VIP B na C na mzunguko itakuwa ni Sh 5,000. Kama Simba itatinga nusu fainali uwezekano wa Tanzania kupanda kwenye viwango vya ubora wa soka kwa upande wa klabu ni mkubwa na itaongezewa nafasi za ushiriki.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz