Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yapata mbinu mpya, kambini kesho

Simba Rekodi Simba yapata mbinu mpya, kambini kesho

Sat, 26 Mar 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Simba inatarajiwa kuingia kambini kesho Jumapili ili kuanza kujifua kwa mazoezi kujindaa na pambano lao la Kombe la Shirikisho Afrika, Kundi D dhidi ya Union Sportive de la Gendarmerie (USGN) ya Niger, huku wakipewa mbinu mpya.

Wekundu hao wataikaribisha USGN Aprili 3 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa katika mechi ya kuamua hatma yao ya kwenda robo fainali ili iandikishe rekodi mpya kwa timu za Tanzania katika michuano hiyo ama irejee kuendelea na Ligi Kuu.

Simba ipo nafasi ya tatu kwa sasa ikiwa na pointi saba ikilingana na RS Berkane ya Morocco wakiifukuzia Asec Mimosas ya Ivory Coast inayoongoza kundi baada ya kila moja kucheza mechi tano, huku USGN ikiburuza mkini na alama zao tano tu.

Kutokana na ugumu wa pambano hilo, kocha Pablo Franco aliwapa mapumziko wachezaji wake kabla ya keshokutwa kurudi kambini kuanza kujifua, huku makocha na wachambuzi wa soka wakiipa mbinu za kupindua meza kundini ikiwa nyumbani.

Makocha na wachambuzi hao walisema benchi la ufundi la klabu ya Simba inatakiwa kuboresha mambo matatu kwa kikosi hicho ili ifuzu robo fainali ya michuano hiyo.

Nyota wa zamani wa kimataifa wa soka na mchambuzi maarufu, Ally Mayay alisema eneo ambalo Pablo anatakiwa kulifanyia kazi kwa sasa ni safu ya ulinzi ambayo imekuwa ikiruhusu mabao ya aina moja katika mechi nyingi.

Mayay alisema, Simba imekuwa ikifungwa mabao ya kutokana na mipira ya krosi au kona sio tu kwenye michuano hiyo, bali hata katika mechi za Ligi Kuu Bara.

Alisema timu nyingi hutumia zaidi mwanya wa mabeki wa pembeni wa Simba, Shomari Kapombe na Mohammed ‘Tshabalala’ Hussein ambao mara kadhaa huwa wanapanda kusaidia mashambulizi.

Alisema shida hutokea pale wanapopanda mbele kushambulia kisha mpira ukaibwa, hapo haraka wapinzani hujibu mashambulizi kwa kupitia pembeni walikoacha mashimo na kulifikia lango la Simba na kupiga krosi zinazoleta matatizo kwa mabeki wa kati wa Simba na kipa wao.

“Kuna mechi Simba iliruhusu mabao kupitia mipira ya kurushwa.. bado kuna tatizo hilo, ni kazi ya kocha Pablo na wenzake kuhakikisha wanaepuka,” alisema.

Alisema lazima kuwe na ‘covering’ wakati mabeki hao wa pembeni wanapokuwa wanakwenda kushambulia na hivyo lazima kuwe na wachezaji wa viungo wanaoweza kuziba mianya ya pembeni.

“Simba ina wachezaji warefu kama Joash Onyango, Kennedy Juma, Henoc Inonga Baka, Pascal Wawa na wengineo ambao wanaweza kucheza mipira hiyo, hata hivyo imekuwa tofauti. Njia bora ni kuzuia washambuliaji wa timu pinzani kutoshambulia,” alisema Mayay.

Aliyewahi kuwa kocha mkuu wa timu ya Taifa ya vijana ya U-17 ya Copa Coca Cola, Abel Mtweve alisema moja ya maeneo ambayo Simba inatakiwa kuyafanyia kazi ni upande wa viungo.

Mtweve alisema mechi dhidi ya USGN ni ngumu kutokana na aina ya wachezaji wa timu hiyo ya Niger kuwa wenye nguvu na pia wana rekodi nzuri ya kufunga.

“Kocha anatakiwa kufanya chaguo sahihi kwa upande wa wachezaji wa viungo ambao ndiyo injini ya timu. USGN nao wanataka kushinda, hivyo lazima wacheze mchezo wa wazi wa kushambulia, hivyo lazima kuwa makini sana eneo la kiungo kwani ndiyo eneo la mipango mingi ya ushindi hufanyika,” alisema Mtweve.

Kocha wa zamani wa Simba, Abdallah Kibadeni alisema wachezaji wote wanatakiwa kuwa makini katika mchezo huo ili kupata ushindi.

“Wachezaji wakumbushwe tu umuhimu wa hiyo mechi, wajengwe kisaikolojia na watambue nafasi yao, klabu na hata kwa nchi kama watafuzu robo fainali,” alisema.

“Manula (Aishi) awe na ‘timing’ nzuri ya kutoka hadi kwenye sita au kubaki golini, azungumze na mabeki wake muda wote, lakini pia mabeki wake makini katika ukabaji, makosa yatawagharimu,” alisema.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz