Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yapania mamilioni ya Samia

Simba Full Return Wachezaji wa Kikosi cha Simba SC

Wed, 15 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Achana na bonasi na ahadi nono za vigogo binafsi ambao wanazishabikia Simba na Yanga, sasa Rais wa nchi, Samia Suluhu Hassan ameingia mwenyewe katika vita ya kuhakikisha timu hizo mbili zinapata ushindi mnono dhidi ya Raja Casablanca na TP Mazembe mwishoni mwa wiki hii baada ya kuahidi kununua kila bao litakalofungwa kwa fedha sh 5 milioni kwa wawakilishi hao wa Tanzania, huku Simba wakionyesha kuchekelea ahadi hiyo.

Baada ya kupoteza mechi zilizopita dhidi ya Horoya na US Monastir ugenini, wawakilishi hao wa Tanzania wanakabiliwa na mechi ngumu nyumbani ambapo Jumamosi, Simba itaikaribisha Raja Casablanca inayoongoza kundi C la Ligi ya Mabingwa Afrika na kesho yake, Yanga itakuwa nyumbani kucheza na TP Mazembe inayoongoza kundi D la Kombe la Shirikisho Afrika na kwa kuhakikisha zinaipa heshima nchi nyumbani, Rais Samia ametangaza noti hizo na hivyo jukumu kubakia kwa nyota wa timu hizo kufumania nyavu ili wazivune fedha za mkuu wa nchi.

Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, alisema jana kuwa ameagizwa na Rais Samia kufikisha ahadi hiyo wa wachezaji wa Simba na Yanga akiamini itawapa motisha ya kuhakikisha wanapata ushindi katika mechi hizo ili kuweka hai matumaini yao ya kutinga hatua ya robo fainali.

Msigwa alisema kuwa ahadi hiyo ya Rais Samia haitoishia katika mechi za mwishoni mwa wiki hii tu, bali zote za mashindano hayo ya kimataifa.

“Na leo nina salamu za faraja kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hajaweka mbali mambo ya michezo. Amenituma nitangaze kwamba kuanzia sasa timu zetu hizi ambazo zinashiriki Kombe la Shirikisho kila goli ambalo litafungwa na Yanga au Simba dhidi ya timu watakazokutana nazo mwishoni mwa wiki, najua wanakuja hapa TP Mazembe na Raja Casablanca kwa hiyo kila bao litakalofungwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, ametangaza kulinunua kwa shilingi milioni tano.”

“Lakini lengo lake pamoja na kufunga mabao ni timu zetu ni lazima zishinde michezo ya wikiendi hii kwa sababu tunahitaji kushinda ili tujiweke katika nafasi nzuri ya kusonga mbele. Anataka timu zifanye vizuri,” alisema Msigwa.

Jana Mkuu wa Idara ya Habari wa Simba, Ahmed Ally alisema kuwa wamepokea kwa mikono miwili ahadi hiyo ya Rais na hayo ni maagizo watayafanyia kazi na yatafungwa mabao mengi kwenye Dimba la Mkapa.

“Tumesikia ahadi ambayo imetolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kupitia kwa Msemaji wa Serikali, Greyson Msigwa, tunaamini kuwa haya ni maagizo na tunamhakikishia kuwa tutafunga mabao mengi Jumamosi hii ni motisha tosha kwa wachezaji,” alisema Ahmed.

Ahadi hiyo ya Rais Samia ni muendelezo wa sapoti kubwa ambayo amekuwa akiitoa kwa sekta ya michezo tangu alipoingia madarakani mwaka 2021.

Agosti 2021, Rais Samia alitangaza kuwa tayari kudhamini mashindano ya soka kwa wanawake ya nchi wanachama wa Baraza la Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) ambapo atakuwa akitoa kiasi cha Dola 100,000 (Sh 233 milioni) kila mwaka kuendeshea mashindano hayo ambayo hayakuwa na mdhamini hapo awali.

Chanzo: Mwanaspoti