Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yamtangaza kocha wake mpya

13182d415216be82b2061da712a9e5bd Simba yamtangaza kocha wake mpya

Mon, 25 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

HATIMAYE uongozi wa klabu ya soka ya Simba kupitia Mtendaji Mkuu, Barbra Gonzalez jana ulimtangaza Didier Gomes da Rosa kuwa kocha mkuu wa timu hiyo akichukua mikoba ya Mbelgiji Sven Vandenbroeck aliyeacha kazi mwanzoni mwa mwezi huu.

Da Rosa raia wa Ufaransa amejiunga na Simba kwa mkataba wa miaka miwili akitokea klabu ya El- Merrikh ya Sudan ambayo aliifundisha kwa mafanikio kabla ya kuvunja mkataba Jumamosi iliyopita baada ya kupata ofa nono ya kujiunga na miamba ya Tanzania Simba.

Baada ya kujiunga na Simba mtihani mkubwa utakaomkabili kocha huyo ni kuhakikisha Simba inavuka hatua ya makundi na kufika mbali kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini pia inatetea ubingwa wake wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara inaoushikilia kwa misimu mitatu mfululizo.

Akizungumza na vyombo vya habari wakati wa kusaini mkataba huo jana, Mtendaji Mkuu wa klabu ya Simba Barbra Gonzalez, alisema kilichowavutia hadi kumchagua kocha huyo ni rekodi zake pamoja na uzoefu mkubwa alionao na soka la Afrika na mafanikio yake.

“Kabla ya kumtangaza Da Rosa tulikuwa na wakati mgumu kutokana na kupokea maombi ya makocha 70 kutoka pande mbalimbali za dunia, lakini mwisho wasiku tulitua kwake kutokana na uzoefu mkubwa alionao na soka la Afrika lakini pia kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa,” Alisema.

Barbra alisema wanaimani kubwa na kocha huyo na ili kuhakikisha anafanya kazi yake kwa ufasaha, kwenye benchi la ufundi wamemwongezea watu wenye uzoefu akiwemo kocha wa makipa raia wa Brazili, Milton Nienov.

Kiongozi huyo mkuu alisema pamoja na imani waliyonayo juu ya kocha huyo ni vyema mashabiki na wanachama wakampa sapoti na nafasi aweze kutumia taaluma yake kuwapa manufaa ya ndani ya uwanja.

Barbra alisema mara nyingi mashabiki na wanachama wamekuwa mstari wa mbele kumtupia kocha lawama pindi inapotokea timu kupoteza mchezo na amewaomba waache tabia hiyo kwani watampima kutokana na makubaliano waliyokubaliana.

Kwa upande wake, Da Rosa aliushukuru uongozi wa klabu ya Simba kwa kumpa heshima kubwa kuwa kocha wao na yeye ataitumia nafasi hiyo kutumia ujuzi wake ili kuwapa furaha na mafanikio katika muda ambao amesaini mkataba.

"Nina furaha sana kuwa hapa na tuna nafasi kubwa ya kufanya mengi pamoja mbeleni kitu cha msingi tuzidishe umoja na mshikamano naamini hakuna kitakachoshindikana," alisema Da Rosa.

Kocha huyo mzaliwa wa Charenton-le-point nchini Ufaransa amejizolea sifa mbalimbali tangu aanze kufundisha soka la Afrika takribani miaka 10 iliyopita.

Rekodi zake

Rekodi zake zinaonyesha mwaka 2013 alitwaa taji la ligi kuu nchini Rwanda akiwa na klabu ya Rayon Sports na msimu wa 2014/2015 alitwaa taji la ligi ya Cameroon akiwa na klabu ya walima pamba ya Cotton Sports Fc.

Baada ya kufanya vizuri nchini Rwanda, mabosi wa Rayon Sports walimuongeza mkataba, jambo ambalo yeye alilikataa kwa kuwa alihisi ameshakamilisha huduma yake nchini humo.

Gomez akajiunga na CS Constantine ya Algeria kwa kandarasi ya miaka miwili na kuiokoa timu hiyo kushuka daraja kwenye ligi hiyo kwakuwa ilikua na hali mbaya.

Machi 2019 alijiunga na Horoya Ac ya nchini Guinea ambapo hakudumu baada ya kufukuzwa Novemba kwa sababu za kiufundi na kwa kupoteza mechi tatu kati ya sita alizocheza na kushinda mbili huku akidroo moja

Januari 8, mwaka jana klabu ya Ismaily SC ikamtangaza Didier Gomez kama kocha wao mpya na aliiwezesha timu hiyo kufika nusu fainali ya kombe la Arab Cup.

Desemba 14, mwaka jana kocha huyo akajiunga na Al Merrikh ya Sudan na kuiwezesha kufuzu katika hatua ya makundi baada kukosa fursa hiyo kwa miaka minne nyuma.

Mafanikio binafsi

ya kocha huyo

-Mwaka 2014 Kocha Bora wa Cameroon

-2015 alikua kocha wa tatu kwa ubora Afrika kwa makocha wa Kifaransa.

Chanzo: habarileo.co.tz