Simba imeingia anga za Azam FC, kuwania saini ya beki wa Yanga, Kibwana Shomari anayemaliza mkataba wake mwishoni mwa msimu huu na bado klabu yake haijafikia mwafaka naye.
Azam FC ndio ilikuwa ya kwanza kumpelekea ofa mchezaji huyo, lakini baada ya Mwanaspoti kuchapisha taarifa hizo, Simba ikaamua kutupa ndoano na siyo mara ya kwanza kumhitaji beki huyo, kwani hata msimu uliopita ilimtaka.
Taarifa kutoka kwa mtu wake wa karibu na mchezaji huyo zinasema ana ofa tatu mkononi mwake ya Yanga, Simba na Azam, hivyo baada ya kuzichambua, alizipa masharti klabu hizo, itakayofanikisha mahitaji yake anaweza akasaini.
"Baada ya kuzisoma ofa, alikuwa na vipengele anavyovihitaji ndani ya timu itakayokuwa tayari kukubaliana navyo, atakuwa tayari kusaini, kwani kazi yake ni soka, kwa sasa anasubili zimrejeshee majibu," kimesema chanzo cha karibu na mchezaji huyo na kuongeza:
"Awali Yanga, ilikaa kimya, baada ya kusikia fununu za anatakiwa na Azam, ikampelekea ofa ya mazungumzo ya mkataba mpya".
Chini ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Nasreddine Nabi kiwango cha Kibwana kilikuwa juu ambapo alicheza nafasi zaidi moja uwanjani yaani kama beki wa kulia na kushoto, lakini baada ya ujio wa Miguel Gamondi na ongezeko la beki wa kigeni, Kouassi Attohoula Yao ambaye ameonyesha kiwango bora kumemfanya asugue benchi.
Yanga ilipocheza dhidi ya Dodoma Jiji, Kibwana baada ya kupewa nafasi, alionyesha uwezo mkubwa utakaomfanya Gamondi kuumiza kichwa kuamua kumbakiza ama kuachana naye.
Wachezaji wengine wanaomaliza mikataba yao Yanga ni Aziz Ki, Zawadi Mauya, Bakari Mwamnyeto, Farid Mussa, Mahlatse Makudubela 'Skudu' na Metacha Mnata.