Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yamkoamlia beki Mcameroon

Che Fondoh Malone Simba yamkoamlia beki Mcameroon

Tue, 27 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mabosi wa Simba wanaendelea kukisuka kikosi chao kimyakimya na wameweka kambi kwa muda nchini Cameroon wakiipigania saini ya beki mmoja wa kazi wa kati, Che Fondoh Malone.

Simba imeshakubaliana kila kitu na Malone ili aje kuimarisha safu yao ya ulinzi kwa msimu ujao lakini ugumu upo kwa klabu yake ya CotonSport ambayo ina mkataba na kitasa hicho.

Malone amebakiza mwaka mmoja kwenye mkataba na klabu yake huku Simba ikisisitiza wakati muafaka wa kumpata ni sasa wakiwa tayari walishawasilisha ofa ya kwanza kwa Wacameroon hao.

CotonSport imegomea ofa ya kwanza ya Simba waliotaka kuwapa Dola 25,000 ili kununua mkataba wake, lakini klabu hiyo imewaambia 'acheni utani fedha kidogo sana hiyo kumpata Malone'.

Malone mwenyewe ameshachanganyikiwa na ofa ya Simba akiwa ameshakubaliana nao kila kitu, huku hatua ngumu ikibaki kwa klabu yake pekee ili kuridhia atua Msimbazi kuvaa uzi mwekundu na mweupe.

Mwanaspoti linafahamu, Malone tayari ameshawagomea klabu yake kuongeza mkataba mpya, huku akiwataka kulegeza masharti yao ili asipishane na ofa ya wekundu hao.

Kocha Roberto Oliveira 'Robertinho' ameshamchanganya beki huyo akimwambia apambane aje kuungana na winga Leandre Willy Onana ambaye tayari ameshasaini mkataba wa miaka miwili na Simba akitokea Rayon Sports ya Rwanda akimaliza msimu kama kinara kwa mabao 16 aliyoyafunga.

Ripoti ya kocha Robertinho, inahitaji mabeki wawili akiwemo mmoja wa kati kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika kwa nia ya kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Mohamed Ouattara na kama atatua itamfungulia mlango, Joash Onyango aliyeomba kuondoka.

Mabosi wa Simba tayari jana Jumapili, walikuwa wanajipanga kuwasilisha ofa ya pili kwa Wacameroon wakiendelea kuipigania saini ya beki huyo.

MALONE AFUNGUKA Akizungumza na Mwanaspoti, Malone alisema anafurahia kuhitajiwa na Simba, ila anasubiri kuona muafaka kati ya klabu hizo mbili, ili maisha yake yawe mepesi Msimbazi.

"Nimeishi hapa (CotonSport) kwa heshima, lakini ni faraja kwangu kuona nahitajika na klabu nyingine kubwa kama ya Simba, ofa zipo nyingi ila nasubiri kuona wapi viongozi wa klabu hii watafikia makubaliano na wenzao wa Simba," alisema Malone anayemudu pia kucheza kama beki wa kulia mwenye umri wa miaka 24.

Hesabu za mabosi wa Simba kwa ubora walioubaini kwa beki huyo ni kuja kutengeneza ukuta mgumu zaidi akishirikiana na Mkongoman Henock Inonga.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: