KIKOSI cha wachezaji 27, benchi la ufundi wataondoka nchini alfajiri ya Jumanne Mei 11, 2021, kwenda Afrika Kusini kuwakabili Kaizer Chiefs kwenye robo fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakaopigwa Jumamosi hii saa 1 usiku.
Simba katika kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye mchezo huo wa ugenini tayari wamewatanguliza kundi lao la kwanza kuweka mazingira vizuri.
Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata tayari Simba miongoni mwa watu ambao wameondoka nchini juzi Jumamosi mara baada ya mchezo wa Yanga, kughairishwa ni Mratibu, Abbas Selemani na mpishi, Samuel Cyprian.
Mratibu huyo atakwenda kusimamia na kuweka sawa mazingira ya msingi kama hoteli ambayo timu itafikia, uwanja wa mazoezi, usafiri, vyakula na mambo mengine.
Msafara huo wa Simba ambao utaondoka nchini si chini ya watu 40, utapanda shirika la ndege la Kenya Airway.
Kutokana na Simba kuondoka nchini leo maana yake mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Coastal Union uliopangwa kupigwa Jumanne saa 1:00 usiku hautakuwepo.
Kocha wa Simba, Didier Gomes alisema baada ya mchezo wa dabi dhidi ya Yanga kushindwa kuchezwa maana yake wanawekeza nguvu katika mechi zilizo mbele yao.
Gomes alisema; “Yaliyopita tumeshayasahau sasa nguvu yetu ni kuona tunakwenda kurahisisha kazi katika mechi ya kwanza ugenini kwani naamini msimu huu ni zamu ya Simba kufanya vizuri na kufika mbali.”
Kikosi cha Simba jana asubuhi kilicheza mechi mazoezi wenyewe kwa wenyewe kuanzia saa 4 ili kujiweka sawa.