Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yajivunia kusajili kikosi cha kizazi kipya

Simba Sc Usajili Simba yajivunia kusajili kikosi cha kizazi kipya

Thu, 18 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Klabu ya Simba imesema idadi ya wachezaji wapya iliyowasajili msimu huu ni wengi zaidi kusajiliwa kwa mkupuo kwa miaka tisa iliyopita, ikisema ilichofanya ni mapinduzi ya kuanza upya, wakiwa na kikosi cha kizazi kipya.

Akizungumza kutoka Ismailia nchini Misri ambako wameweka kambi kwa ajili ya msimu mpya wa mashindano, Mratibu wa timu hiyo, Abbas Ally, alisema hata yeye hajawahi kuona Simba ikisajili wachezaji wengi wapya kwa mkupuo mmoja, hivyo inaonyesha kuwa viongozi wa klabu hiyo, akiwamo Mwekezaji, Rais wa Heshima na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mohamed 'Mo' Dewji, wamedhamiria kuijenga timu mpya kabisa.

"Usajili huu una maana kubwa sana katika kikosi cha Simba kwa sababu tangu 2015, hakujawahi kufanyika mabadiliko makubwa kwenye kikosi kama mwaka huu. Mimi niko hapa tangu 2015, sijawahi kuona kitu kama hiki, kwa hiyo haya ni mapinduzi na huu ni mwanzo mpya.

"Watu wanataka kuona Simba yao ile ambayo wameizoea, ile ambayo inamiliki sana mpira, inamiliki mchezo kwa kiasi kikubwa na kuwapa wakati mgumu wapinzani na iliyokuwa inafanya vizuri karibuni kila mchezo, ikiwamo kupata makombe karibuni yote yanayokuwa mbele yao," alisema Abbas.

Alisema kwa miaka mitatu iliyopita wanachama na mashabiki wa klabu hiyo hawakuwa na furaha kutokana na kikosi chao kutokukuwa kwenye kiwango kisichoridhisha na kutopata matokeo, hivyo imewasukuma viongozi kufanya mabadiliko kama hayo. Aliwatoa wasiwasi baadhi ya mashabiki ambao wanaona kuwapo kwa wachezaji wengi kutachelewesha muunganiko wa wachezaji.

"Unajua matokeo ya misimu mitatu imewavunja sana watu mioyo yao, tulijaribu kukijenga kikosi, lakini timu ilikuwa haichezi vizuri na matokeo hayakuwa mazuri, ndiyo maana wanahofu wingi wa wachezaji wengi waliosajiliwa kama wanaweza kuunganika kwa muda mfupi, wana haki, lakini nadhani tukiwa tunapata ushindi kwenye michezo yetu hayo yote watayasahau," alisema mratibu huyo.

Alisema haamini kama watachukua muda mrefu kutokana na umahiri wa benchi la ufundi lililopo na umri mdogo wa wachezaji ambao ni rahisi kushika maelekezo.

"Ukiangalia mchanganyiko wa wachezaji tulionao ni vijana, wana umri mdogo, ni wepesi kushika maelekezo, ni timu ya kizazi kipya, mimi naamini baada ya mwezi tu, aina ya benchi la ufundi tulilonalo na aina ya wachezaji tulionao, tupakuwa na kikosi bora sana na watu wataamini kuwa katika soka kila kitu kinawezekana hata kwa muda mfupi," alisema.

Simba imesajili jumla ya wachezaji 13 wapya, saba wageni na sita wazawa. Wachezaji wa kigeni ni Jushua Mutale, Steven Mukwala, Jean Charles Ahoa, Debora Fernandes Mavambo, Augustine Okajepha, Valentin Nouma na Karaboue Chamou.

Wazawa ni, Lameck Lawi, Abdulrazack Hamza, Valentino Mashaka, Omari Omari, Kelvin Kijili na Yusuph Kagoma. Hata hivyo, kwa mujibu wa Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, Crescentius Magori, bado usajili unaendelea, hivyo idadi itaongezeka.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live