Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yajiondoa kwa Mpanzu, kipa wa Horoya atua

Mo Dewji X Mpanzu Simba yajiondoa kwa Mpanzu, kipa wa Horoya atua

Mon, 29 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Klabu ya Simba imejiondoa kwenye dili la kutaka kumsajili winga wa AS Vita Club, Elie Mpanzu, kwa kile ilichobaini kuwapo kwa udanganyifu mwingi, huku mchezaji huyo sasa akijiandaa kutimkia Ubelgiji kwenye Klabu ya KRC Genk.

Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema viongozi wa Simba wameamua kukata mawasiliano baada ya kuwapo kwa watu wengi wanaojitaja kama mameneja, huku kila mmoja akidai ndiye mwenye mamlaka na mchezaji huyo, kitu ambacho kimesababisha kuchelewa kumsajili na kujiunga na wenzake kambini nchini Misri.

"Viongozi wa Simba wamefanya kila jitihada, dili lilikuwa likamilike zamani sana, kama utakumbuka awali ilipeleka ofa ya dola 200,000 za Kimarekani, lakini klabu yake ilikataa na ikahitaji 250,000.

"Viongozi hawakuendelea na dili hilo, lakini baada ya kuondoka kwa Kibu Denis walirejea tena na kiasi ambacho alihitaji mara ya pili, lakini bado kumekuwa na mkanganyiko, klabu inahitaji pesa, klabu yake ambayo alianzia kucheza soka nao wanahitaji.

"Pia kuna mameneja kadhaa ambao baada ya kuona dili hilo nao wamejitokeza, sasa viongozi wameamua kuwakatia simu wote, ukweli ni kwamba usajili wa Mpanzu una uongo mwingi, msimamizi halali wa Mpanzu hajulikani, hivyo wamekwepa matatizo," kilisema chanzo hicho.

Chanzo hicho kimesema huenda Simba wakaingia tena sokoni kusaka winga wa kulia kuziba nafasi ya Kibu ambaye ametorokea nchini Norway, huku suala lake likionekana haliwezi kumalizika hivi karibuni kwani kama si kumuuza bei inayotaka klabu hiyo, basi kutoa adhabu kwa mchezaji na kuishtaki klabu iliyomrubuni.

Habari zinasema tayari Mpanzu alishakubali kujiunga na Simba aliyetarajiwa kulipwa mshahara wa Sh. milioni 26 za Kitanzania na ada ya usajili Sh. milioni 323 za Kitanzania.

Kutokana hilo, mchezaji huyo anatarajiwa kutimkia Klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji baada ya dili hilo kushindikana.

Wakati hayo yakiendelea, golikipa mpya wa timu hiyo, Moussa Panpin Camara, alitarajiwa kutua nchini jana mchana kwa ajili ya kusaini mkataba wa kujiunga na timu hiyo.

Picha zilizotolewa jana na vyombo vya habari na mitandaoni nchini Guinea, zilimwonyesha akiwa na mabegi yake Uwanja wa Ndege nchini humo tayari kwa safari ya kuja nchini.

Kipa huyo wa Timu ya Taifa ya Guinea, anatokea Klabu ya Horoya FC nchini humo, na anakwenda kuchukua nafasi ya Ayoub Lakred ambaye taarifa zinaeleza aliumia akiwa kwenye maandaliazi ya msimu mpya nchini Misri.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live